Raia wa Uingereza mbaroni kwa Bhangi

Misokoto ya Bhangi

Na Mwandishi Wetu, Thehabari, Mwanza

MENEJA wa Kampuni ya OTS ya mkoani Shinyanga, ambaye ni raia wa Uingereza  anashikiliwa na Jeshi la Polisi Jijini hapa baada ya kudaiwa kupatikana na misokoto minne ya dawa za kulevya aina ya bhangi kwenye gari analotumia.

Meneja huyo, Hilton Millers (28) alikamatwa juzi majira ya saa 9 mchana katika Hoteli ya Tilapia Kapripoint jijini Mwanza akiwa kwenye gari T 848 ATM aina ya Toyota Land Cruiser.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa leo, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Simon Sirro alisema Millers ambaye ni meneja wa OTS inayojihusisha na uuzaji wa matairi za magari mikoa ya Mwanza na Shinyanga, anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho.

“Meneja huyo ni raia wa Uingereza, nimeambiwa sasa hivi bado anahojiwa na kuchukuliwa maelezo, kesho tutamfikisha mahakamani,” alisema Sirro.

Aidha aliendelea kuwa Millers alikamatwa na askari wa doria akiwa katika eneo la Hoteli ya Tilapia na alipopekuliwa alikutwana misokoto hiyo ya bangi na alipohojiwa alikiri kuvuta dawa hizo za kulevya, hivyo atafikishwa mahakakani baada ya taratibu za kipolisi kukamilishwa.