WANAMICHEZO wa Afrika na Ghana wamempoteza kiongozi makini na mahiri wa michezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Ghana, John Evans Atta Mills kuliko pengine makundi mengine ya rais.
Alikuwa mwanamichezo, kiongozi wa michezo na shabiki wa michezo ukiwamo mchezo wa soka ambako alikuwa mfuasi maarufu wa klabu ya soka la Hearts of Oak ya mjini Accra, Ghana.
Rais wa Ghana kwa karibu miaka minne iliyopita alikuwa kiongozi wa michezo wa miaka mingi na mwanamichezo mahiri na wakati akiwa mhadhiri kwenye Chuo Kikuu cha Ghana, Legon, kwa karibu miaka 30, John Evans Atta Mills pia alikuwa kiongozi wa michezo.
Alikuwa mpenzi wa michezo na alikuwa Rais wa Klabu ya Michezo ya Chuo Kikuu cha Ghana kwa miaka 20 mfululizo, na kwa miaka 10 alikuwa Rais wa Chama cha Michezo cha Vyuo Vikuu Vyote vya Ghana.
Rais Mills alishiriki katika michezo mingi kama mchezaji katika maisha yake. Lakini mchezo wake mkuu ulikuwa ni mpira wa magongo. Alikuwa “mlevi” wa mchezo huo ambako alichezea timu ya taifa ya mchezo huo ya Ghana.
Kwa hakika akiwa Makamu wa Rais kwa miaka minane, John Evans Atta Mills aliendelea kuchezea timu ya wazee ya Ghana. Aliichezea timu hiyo akiwa Makamu wa Rais kwa miaka minane, na akiwa Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani katika Ghana kwa miaka minane kati ya 2001 na 2008 kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi.
Alikuwa msemaji mkuu wa shughuli za michezo na ushiriki wa michezo. Alikuwa mwanamichezo makini na mpenzi mkuu wa michezo. Rais Mills alishiriki katika kukijenga Chama cha Mpira wa Magongo cha Ghana, Baraza la Michezo la Ghana, na timu ya soka maarufu ya Ghana, Accra Hearts of Oak Sporting Club.