Mbowe aachiwa huru, ulinzi mkali watawala

 

Na Janeth Mushi, Thehabari, Arusha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha jana mjini hapa imemfutia hati ya kukamatwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe, hati iliyokuwa imetolewa na Mahakama hiyo.

Mbele ya Hakimu Mfwidhi wa Mahakama hiyo, Charles Magessa Mahakama pia imemuondoa mdhamini wa Mwenyekiti huyo baada ya kushindwa kutokea mahakamani kutokana na kukabiliwa na kesi katika mahakama ya Mwanzo ya Maromboso mjini Arusha.

Aidha kuondolewa kwa mdhamini huyo kumefuatia baada ya kujitetea kuwa alishindwa kufika mahakamani Mei 27, 2011 kwa madai kuwa siku hiyo alikuwa akihudhuria kesi inayomkabili katika Mahakama ya Mwanzo na  alichelewa kutoka hali ambayo ilimshinda kuhudhuria mahakamani.

Baada ya mdhamini huyo kutoa maelezo hayo, Magessa alimtaka aeleze sababu za kutofika mahakamani hapo siku ya Mei 30, ambapo alidai alikuwepo mahakamani siku hiyo na hakuitwa kutoa hudhuru wa mshitakiwa wake hadi kesi hiyo ilipoahirishwa.

Magessa alimtaka mshitakiwa huyo aoneshe chumba kipi kilitumika kusikiliza kesi hiyo, ambapo alishindwa kukitambua hivyo, hakimu kumtaka mshitakiwa Mbowe kutafuta mdhamini mwingine kwa kuwa aliyenaye anakabiliwa na kesi yake inayomsababisha ashindwe kutimiza masharti ya udhamini.

Pia Magessa alisema sababu ya pili iliyotolewa na mdhamini ya kuwa alikuwepo mahakamani hapo siku ya Mei 30 si ya kweli na kwamba ameidanganya mahakama kwakua hata wakili wake aliieleza mahakama kuwa siku hiyo hakuwepo mshitakiwa wala mdhamini wake.

Kutokana na agizo hilo upande wa mashtaka ulitimiza agizo hilo kwa kumteua Diwani wa Kata ya Elerai, John Bayo kuwa mdhamini wake mpya kwa masharti ya kumkumbusha mshtakiwa kufika mahakamani na kama ana hudhuru yeye afike bila kukosa.

Kwa upande wake wakili wa upande Serikali, Juma Ramadhan alidai ingekuwa vizuri mshtakiwa akafutiwa dhamana ili apatikane kila anapohitajika mahakamani hapo, hata hivyo alikuwaliana na uamuzi wa mahakama kufuta hati ya kukamatwa kwa Mbowe pamoja na mdhamini ila wapewe onyo kali ili wasirudie kosa la kudharau amri ya Mahakama.

Kwani alidai kuachia vitendo kama hivyo kuendelea vitasababisha washtakiwa wengine kupuuza Mahakama na kusababisha kesi hiyo kuchukua muda mrefu kumalizika kutokana na wahusika kutohudhuria.

Madai hayo ya Wakili wa Serikali yalipingwa vikali na wakili anayewatetea washtakiwa hao, Method Kimomogolo kwa maelezo kuwa mshtakiwa alikuwa na ruhusa ya Mahakama kuhudhuria vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge na haikufahamika kama mdhamini alipaswa kufika mahakamani hapo.

Aidha Kimomogolo aliiomba mahakama kuwapa ruhusa washtakiwa ambao ni wabunge kutohudhuria mahakamani Juni 24 ili waweze kuhudhuria kikao cha bunge cha kujadili bajeti kilichoanza leo mjini Dodoma.

Kufuatia ombi hilo Magessa pamoja na wakili wa Serikali walikubaliana na ombi hilo kwa masharti kuwa wakili wao pamoja na washtakiwa ambao si wabunge kufika mahakamani hapo kesi itakapo tajwa kwa ajili ya uamuzi utakaotolewa.

Washtakwia wabunge walioombewa ruhusa hiyo ni pamoja na Mbowe Mbunge wa Hai, Phillemon Ndesamburo wa Moshi Mjini, Godbles Lema wa Arusha Mjini na Joseph Selasini wa Rombo.

Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni alifikishwa mahakamani hapa majira ya saa 2:18 asubuhi na gari linalotumiwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Leonard Paul aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa na namba za usajili T 322 BGT chini ya ulinzi mkali wa maofisa wa polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam akiwemo, Duan Nyanda na wengine wa mjini hapa.

Mbowe na wenzake 18 wanakabiliwa na kesi ya kufanya maandamano yasiyo na kibali na kusababisha vifo vya watu watatu mnamo Januari 5 mwaka huu, ambapo wanatetewa na wakili, Kimomogolo na Albert Msando wakati upande wa Serikali ukiwakilishwa na mawakili Juma Ramadhan na Edwin Kakolaki.

Aidha katika mahakama hiyo iliyokuwa imefurika mamia ya wakazi wa jiji la Arusha baadhi ya wabunge wa CHADEMA akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Kabwe Zitto, Halima Mdee (Kawe), Ezekiel Wenje (Nyamagana), Joseph Selasini (Rombo) na Joseph Mbilinyi (au Mr
II wa Mbeya Mjini), Israel Nase (Karatu) na Godbless Lema (Arusha Mjini).

Wengine ambao ni wabunge wa Viti Maalumu ni Grace Kiwelu(Kilimanjaro), Paulina Geluk (Babati), Lucy Owenya, Joyce Mukya (Arusha), Suzan Lyimo (Kilimanjaro), Suzan Kiwanga (Morogoro), Christine Lissu(Singida) na Rahya Ibrahim (Pemba).

Aidha nje ya mahakama hiyo magari yaliyokuwa na Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) yalikuwa yamezunguka mahakama hiyo huku askari hao pia wakiwa wamewekwa katika baadhi ya maeneo ya jijini hapa.