Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi 16 na wageni wengine wengi maarufu, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, kushiriki mazishi ya aliyekuwa Rais wa Ghana, John Evans Atta Mills Agosti 10, 2012, mjini Accra.
Rais Kikwete na ujumbe wake anatarajiwa kuwasili mjini Accra, mji mkuu wa Ghana, adhuhuri ya Agosti 9, 2012, kuhudhuria mazishi ya kiongozi huyo aliyefariki dunia mchana wa Jumanne, Julai 24, 2012 kwa ugonjwa wa kansa ya koo kwenye Hospitali ya kijeshi inayoitwa 37 Military Hospital mjini Accra.
Rais Mills ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 69 anatarajiwa kuzikwa kwenye makaburi yaliyoko eneo la bustani la Geese kwenye Mtaa wa Castle Drive karibu na Hekalu ya Osu mjini Accra baada ya kuwa mwili wake umeagwa kwenye shughuli maalum itakayofanyika kwenye bustani ya Independence Square kesho Ijumaa.
Rais Mills ambaye nafasi yake imechukuliwa na Rais John Dramani Makama atazikwa katika kaburi lililojengwa na kampuni ya ujenzi ya Serikali ya China ya HL Construction. Mwili utazikwa baada ya kupitishwa katika mitaa maarufu ya jiji la Accra ili kutoa nafasi ya mwisho kwa wananchi wa Ghana kuuona na kuuaga mwili huo kwa mara ya mwisho.
Agosti 8, 2012, mwili wa Mills ulihamishwa kutoka kwenye Hospitali ya 37 ya Jeshi la Ghana ambako umekuwa umehifadhiwa tokea kufariki dunia na kupelekwa kwenye nyumba ya familia iliyoko katika Barabara ya Spintex kwa ajili ya kufanyiwa taratibu za mila.
Baada ya shughuli hiyo, mwili wa Mills ulihamishiwa kwenye jumba la kulia la Ikulu ya Ghana ambako wananchi wamekuwa wanatoa salamu zao za mwisho kwa mwili wa kiongozi wao. Mwili wa Rais Mills utabakia katika sehemu hiyo mpaka utakapohamishiwa Independence Square kwa ajili ya shughuli ya mazishi.
Miongoni mwa watu waliotoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Rais leo ni pamoja na Rais John Kuffor ambaye Rais Mills alichukua madaraka kutoka kwake. Vikundi vya muziki na vikundi vya utamaduni viliendelea kutumbukiza Ikulu siku nzima jana na usiku kucha.