Watendaji wa vijiji kuwasaka wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu

Na Mwandishi Wetu, Same

SERIKALI wilayani Same mkoani Kilimanjaro imewataka watendaji wa kata na vijiji kuwasaka wazazi wanaoendeleza vitendo vya kikatili vya kuwaficha watoto wenye ulemavu ili wachukuliwe hatua.

Tamko hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi alipokuwa akipokea msaada wa vyandarua sanjari na kuzindua utumiaji wa vyandarua vilivyo tiwa dawa kwenye kituo Cha Mother Kevina Hope kinacho hudumia watoto wenye ulemavu.

Alisema zaidi ya watoto 200 wenye ulemavu walioko katika wilaya hiyo wamekuwa wakifichwa na wazazi wao hali ambayo imekuwa ikiwafanya kukosa haki za kimsingi ikiwemo elimu.

Alisema kwa sasa hali hiyo ambayo inaonekana kuwa ya kikatili kwa watoto hao, inapaswa kukomeshwa hivyo ni vema watendaji wa kata na vijiji wakawafuatilia na kuwakamata wazazi wenye tabia hiyo ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Aidha alisema ni lazima jamii itambue kuwa watoto wenye ulemavu ni watoto kama watoto wengine na wanayo haki ya kupatiwa elimu pamoja na mahitaji mengine yanayowahusu watoto na si mkosi au balaa kama ilivyojengeka katika maeneo mengi.

“Ni lazima tufike mahali sasa tuondokane na dhana potofu ambazo zimejengeka miongoni mwa jamii nyingi kuwa mtoto mlemavu ni mkosi katika familia, watoto hawa ni watoto kama ilivyo watoto wengine na wanahitaji kutimiziwa mahitaji yao yote ya kimsingi ikiwemo elimu na katika hili sasa naomba watendaji tulifuatilie ili tulikomeshe,” alisema Kabufi.

Akizungumza mlezi wa kituo hicho cha watoto wenye ulemavu, Febronia Paul alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya vyoo kwa watoto wenye ulemavu kutokana vyoo vilivyopo kwa sasa kutokidhi mahitaji yao hivyo kuwasababishia usumbufu mkubwa.

Alisema pamoja na changamoto zinazowakabili kituoni hapo, wazazi wenye watoto walemavu bado hawajahamasika vya kutosha kuwapeleka watoto wao shule, jambo ambalo ni tatizo kubwa na limekuwa likiwafanya watoto hao kuwa mzigo na tegemezi katika jamii.