Serikali kufidia N’gombe waliouawa Maswa

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu akizungumza na wafanyakazi na viongozi wa pori la akiba Maswa.

Na.Nathaniel Limu

Serikali imeahidi kutoa kiasi cha Milinioni sita kulipa fidia ya ng’ombe 22 wanaodaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori wa pori la Akiba Maswa wilayani Meatu, mkoani Simiyu.

Inadaiwa ng’ombe hao walipigwa risasi na kuuawa Desemba 2009 baada ya kuingizwa kuchungia ndani ya hifadhi hiyo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria zinazolinda hifadhi za wanyama pori .

Ahadi hiyo imetolewa juzi na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wakazi wa kata ya Sakasaka jimbo la Kisesa.

Alisema lengo la uamuzi huo ni kuimarisha mahusiano mazuri kati ya Askari wa wanayamapori na Wakazi wa vijiji vinavyozunguka akiba ya pori hilo.

“Pia ni sehemu ya mikakati inayochukuliwa na Serikali ya kuhakikisha mgogoro wa muda mrefu kati ya uongozi wa pori la akiba Maswa na wananchi wakazi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo,unamalizika na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo,” alisema Nyalandu.

Katika hatua nyingine, Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Singida kaskazini, alisema kuwa Serikali inatarajia kuunda kamati huru ambayo itashughulikia kutafuta ufumbuzi wa mgogoro uliopo kwa muda mrefu katika akiba ya Pori la Maswa.

“Katika kamati hii,kutakuwepo na Mwakilishi mmoja kutoka wizara ya maliasili na utalii na wajumbe watakaobaki watakuwa ni watu huru ambao watazitendea haki pande zote mbili. Ni matarajio yetu kwamba taarifa itakayotolewa na kamati hiyo haitaonea au kupendelea upande wowote, itakuwa timilifu,” alifafanua naibu waziri huyo.

Nyalandu alisema kamati hiyo itatoa taarifa yake wizarani mapema kabla bunge la sasa kuhairishwa.

Katika hatua nyingine, alitumia fursa hiyo kuagiza wananchi waendelee kuelimishwa vya kutosha juu ya sheria zote za hifadhi za wanyama pori ili waweze kuzitii bila ya kushurutishwa.

“Napenda kukumbusha kuwa marufuku kuchungia,kulima,kuingiza au kufanya shughuli zo zote za kijamii ndani ya hifadhi la wanyama pori. Mfugaji au mtu yeyote atakayevunja sheria halali zilizowekwa atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Nyalandu.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini, alisema hifadhi ya Pori la akiba Maswa ipo kwa mujibu wa sheria.

“Kwa hiyo, wananchi kuigiza mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo kwa madai ya kutokuwa na maeneo ya malisho ni kuvunja sheria. Tunashauri wananchi wenye mifugo wanaopakana na pori la akiba la Maswa watafute maeneo mengine ya kupeleka makundi yao ya mifugo, au washauriwe kupunguza mifugo yao kwa kuanzisha ufugaji wa kisasa,” alisema DC Kirigini.

Aidha, alisema kuwa wataendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa madai kwamba hifadhi zilizopo, ni hazina kwa Vizazi vilivyopo sasa na vya baadaye kwa Nchi ya Tanzania na dunia kwa ujumla.

Wakati huohuo, DC Kirigini ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kubadilisha jina la akiba la pori la Maswa na kulipa jina la akiba ya pori la Meatu.

Alisema kuwa kwa vile sasa wilaya ya Maswa imegawanywa na kuwa na wilaya wilaya tatu baada ya kuanzishwa kwa wilaya ya Bariadi na Meatu,akiba ya pori hilo ambalo sehemu kubwa ipo wilaya mpya ya Meatu,hivyo kuna ulazima wa kuitwa pori la akiba la Meatu.

Kwa upande wake Nyalandu alisema ombi hilo la kubadilisha jina la pori hilo linazungumzika.