Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete usiku wa leo, Ijumaa, Agosti 3, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Dk. Idris Jala, Waziri wa Nchi na Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Utendaji wa Serikali ya Malaysia (PEMANDU) katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia na ujumbe wake.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Ndogo mjini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue, Waziri Jala amemweleza Rais Kikwete siri ya mafanikio ya Malaysia katika kutekeleza Mpango wa Mageuzi.
Jala na ujumbe wake wa watu 10 uko nchini na mjini Dodoma kushiriki katika Warsha ya Utekelezaji, Ufuatiliaji na Kutathmini Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano. Warsha hiyo ya siku mbili imepangwa kuanza kesho, Jumamosi, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mtakatifu Gaspar mjini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemweleza kuhusu matumaini na matarajio ya Serikali ya Tanzania kuhusu warsha hiyo hasa katika kuibua njia bora zaidi za utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Rais Kikwete amesema kuwa njia hizo zitakuwa ni pamoja na kuwa na mpango wa utekelezaji, muda wa kutekeleza mipango hiyo na bajeti ya utekelezaji wa mipango hiyo.
Dk. Jala amesema kuwa ili mpango wowote mzuri wa mageuzi ufanikiwe ni lazima uongozwe kutoka kwenye ngazi ya juu kabisa ya Serikali. “Ni sawa na ujenzi wa nyumba. Anakuwepo mchoraji wa nyumba, mjenzi na msimamizi wa ujenzi, lakini hatimaye mjenzi mkuu ni mwenye nyumba mwenyewe.”
Kuhusu ukosefu wa fedha za kutosha za kutekeleza kikamilifu mipango ya maendeleo, Dk. Jala amesema kuwa katika maisha zipo pesa za kutosha kutekeleza mipango iliyoandaliwa, ili mradi mipango yenyewe ilenge katika kutekeleza mambo machache muhimu.