Majambazi wavamia na kuua wawili

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Said Mwema

Na Mwandishi Wetu, Moshi

WALINZI wawili wa Kambi ya Mountain Side wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, wamefariki dunia baada ya kuvamiwa na kupigwa na watu waodhaniwa kuwa majambazi, kisha kuvunja stoo na kuiba mali.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Robert Boaz amesema tukio hilo limetokea Agosti 3 majira ya saa Nane na robo usiku eneo la Olmoloq Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro. Kambi hiyo inamilikiwa na mwekezaji, Lucas Edward (46) raia wa Uingereza. Kamanda Boaz alisema miongoni mwa mali zilizoibwa ni dawa za kilimo za aina mbalimbali, Solar Paneli na mkokoteni.

Kamanda Boaz alisema watu hao waliouawa ambao ni walinzi katika kambi hiyo ya Mount Side walivamiwa na watu hao ambao bado hawajafahamika na kushambuliwa hadi kufa sehemu mbalimbali za miili yao kwa Mawe hali ambayo iliwasababishia kupata majeraha makubwa sehemu za kichwani.

Kamanda Boaz aliwataja waliouawa kuwa ni Sadick Rashid (35) na Dunia Said (40)ambapo wote ni walinzi katika kambi hiyo ya mwekezaji. Aidha kamanda Boaz alisema kufuati tukio hilo jeshi la polisi kwa kushirikiana na vikosi mbalimbali vya polisi pamoja na mbwa limeanzisha msako mkali kuwatafuta wahalifu hao ili kuwatia mikononi mwa sheria.

Kamanda Boaz alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mbalimbali za kiuhalifu na wahalifu ikiwa ni pamoja na kuwafichua wale wote ambao wanajihusisha na biashara ya wahamiaji haramu kwa kuwasafirisha au kuwahifadhi.