Wahamiaji haramu 39 wanusurika kifo

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz

Na Mwandishi Wetu, Moshi

WAHAMIAJI haramu 39 kutoka nchini Somalia wamenusurika kufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.

Wahamiaji hao ambao inaelezwa walikuwa wakitokea maeneo ya Taveta nchini Kenya, eneo ambalo waliingia nchini Tanzania kinyume cha sheria walinusurika kufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonga kingo za daraja katika Mji mdogo wa Himo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Kamanda huyo alisema tukio hilo lilitokea Agosti 3 majira ya saa 11:45 alfajiri katika barabara ya Moshi-Himo eneo la daraja la Kilimapofo Himo.

Kamanda boaz alisema wahamiaji hao walipata ajali wakati wakisindikizwa na Askari baada ya kuwakamata katika eneo la Mabungo nje kidogo ya manispaa ya Moshi wakiwa wanawapeleka katika kituo kidogo cha polisi cha Himo. Kamanda alisema wahamiaji hao walikamatwa wakiwa na Gari lenye namba za usajili T958 ARB Mitsubish Canter lililokuwa likiendeshwa na John Peter Omary ambaye ndiye mmiliki wa gari hilo.

Aidha kamanda alisema kati ya wahamiaji hao 39 waliopata ajali 27 wamejeruhiwa na kwa sasa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya KCMC huku wengine 12 wakiwa hawajaumia. Kamanda alisema dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo ambaye ndiye mmiliki Peter Omary anashikiliwa na polisi na kwamba uchunguzi unafanyika ili kubaini wahamiaji hao walikuwa wakielekea wapi.

Wakati huo huo jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia wahamiaji haramu Watano Raia wa nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria. Kamanda Boaz alisema Raia hao wa Ethiopia walikamatwa vichakani maeneo ya Kilacha Himo wakati wakisubiria usafiri.