BINGWA wa michuano ya BancABC Super 8 inayoanza Agosti 5 mwaka huu katika miji ya Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza na Arusha atapata sh. milioni 40 wakati makamu bingwa sh. milioni 20. Pia timu mbili zitakazoishia hatua ya nusu fainali kila moja itapata sh. milioni 15 wakati zilizobaki kila moja itapata sh. milioni 5.
Timu zimepangwa katika makundi mawili ya A na B. Kundi A lina timu za Simba (mabingwa wa Tanzania Bara), Jamhuri, Zimamoto na Mtende zote za Zanzibar. Kundi ni Super Falcon (mabingwa wa Zanzibar), Azam, Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro zote za Tanzania Bara.
Mechi za ufunguzi ni Agosti 5 mwaka huu ni Simba vs Jamhuri (Dar es Salaam), Zimamoto vs Mtende (Mwanza), Mtibwa Sugar vs Polisi Morogoro (Arusha) na Super Falcon vs Azam (Zanzibar). Awali mashindano yalikuwa yaanze Agosti 4 mwaka huu lakini yamesogezwa mbele kwa siku moja.
Hatua ya makundi itamalizika Agosti 12 mwaka huu. Mechi za nusu fainali na fainali zote zitachezwa Dar es Salaam. Nimeambatanisha ratiba. Mdhamini banc ABC atagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi kingine, malazi na jezi. Yanga imejitokea kwenye mashindano hayo na nafasi yake imechukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Vodacom.
Wakati huo huo; Kozi ya Uongozi na Utawala ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) itafanyika Msimbazi Center jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 6-11 mwaka huu ikiwa na washiriki 30.
Washiriki wa kozi hiyo itakayonedeshwa na wakufunzi kutoka FIFA ni viongozi kutoka TFF, Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, klabu za Ligi Kuu na viongozi wa mpira wa miguu wa wanawake.
Walioteuliwa kushiriki ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, Rais wa ZFA Amani Makungu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF; Ahmed Mgoyi, Blassy Kiondo, Stanley Lugenge, Khalid Abdallah, Hussein Mwamba na Eliud Mvella.
Wengine ni Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Salum, Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai, wenyeviti wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kagera (Jamal Malinzi), Dodoma (Nassoro Kipenzi) na Pascal Kihanga (Morogoro).
Makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Mara (Mugisha Galibona), Mtwara (Vincent Majiri), Morogoro (Hamisi Semka), Kagera (Salum Chama), Tanga (Beatrice Mgaya) na Dodoma (Stuart Masima). Pia yumo Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Hilal na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga.
Washiriki wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, Ofisa Habari, Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Masoko na Matukio, Jimmy Kabwe, Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba, Ofisa Sheria wa TFF, Neema Lucumay, Ofisa wa Mpira wa Miguu wa Wanawake, Grace Buretha, Amina Karuma (Mpira wa miguu wa wanawake) na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa.