Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Kanisa la ELIM Pentekoste Tanzania, Askofu Peter Liyema Konki kuomboleza kifo cha aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Marehemu Ayoub Enzi Mgweno kilichotokea nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili tarehe 29 Julai, 2012 kutokana na ugonjwa wa Saratani.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mtumishi wa Mungu, Askofu Ayoub Enzi Mgweno kutokana na ugonjwa wa Saratani”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza,
“Ninatambua kwamba hata baada ya utumishi wake wa kuwachunga vyema Kondoo wa Bwana, Marehemu Askofu Ayoub, enzi za uhai wake, aliendelea kuwa Mtumishi wa Kanisa la ELIM Pentekoste Tanzania kama Mchungaji, hivyo ni dhahiri kwamba kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa Waumini wa Kanisa hilo popote walipo”.
Katika maisha ya utumishi wake, Askofu Ayoub Enzi Mgweno aliwatumikia Waumini wa Chalinze na baadaye Tanga kabla ya kustaafu mwaka 2002 akiwa na cheo cha Askofu. Marehemu pia aliwahi kulitumikia Kanisa lake kwa cheo cha Mwenyekiti wa Makanisa ya ELIM Jimbo la Afrika Mashariki na Kati, na ni miongoni mwa Waasisi wa Kanisa hilo hapa nchini.
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Baba Askofu Peter Liyema Konki Salamu za Rambirambi na pole nyingi kwa kumpoteza Askofu Ayoub Enzi Mgweno. Aidha kupitia kwako ninatoa pole kutoka dhati ya moyo wangu kwa Familia ya Baba Askofu Mgweno kwa kuondokewa na mhimili muhimu na nguzo yao”, ameongeza Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahali pema peponi Roho ya Marehemu Askofu Ayoub Enzi Mgweno.
Amewahakikishia Waumini wa Kanisa la ELIM Pentekoste Tanzania pamoja na Familia ya Marehemu kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza Msiba huu. Kwa upande mwingine, Rais Kikwete amewataka wanafamilia ya Marehemu wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, kwani yote ni Mapenzi yake Mola.