Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga
ULE mtindo wa baadhi ya wa kuibuka na kudai wameotesha na Mungu wakiwa usingizini waje kutoa dawa maarufu kama ‘kikombe’ kwa wagonjwa wa magonjwa sugu umeendelea na sasa mganga mwingine kaibuka wilayani Mpanda Mkoa wa Rukwa na kudai ameoteswa na Mungu kufanya kazi hiyo.
Bujukano Charles Shashi (44), mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Usevya ameibuka na kudai kaoteswa kama ilivyo kuwa kwa Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapila wa kijijini Samunge, Loliondo ambaye amejipatia umaarufu mkubwa.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Usevya, Mbasa Kugosora, alisema mganga huyo wa kiyenyeji, Shashi, ameibuka na kudai ni kweli ameoteswa kama Mwasapila na sasa tayari ameanza kutoa dawa hiyo.
Ofisa Mtendaji huyo alisema mganga huyo ambaye kwa muda sasa amekuwa akijishughulisha na uganga wa kiyenyeji, kwa sasa wanakusanyika kwake na anaendelea kutoa huduma hiyo kama ‘babu’ wa Loliondo.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Betty Kipande, alisema watu mbalimbali wamekuwa wakimiminika kila kukicha kwenda kwa mganga huyo kwa ajili ya kupata tiba ya kikombe na kwamba wao hawawezi kuzuia kwa sababu alikuwa mganga tangu zamani zamani.
Alisema kuwa hata hivyo hawawezi kuthibitsha kama dawa hiyo ni kweli inatibu magonjwa sugu kama anavyodai mganga huyo na kuongeza kuwa anayetakiwa kuthibitisha jambo hilo ni Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Sisi hatuwezi kumzuia kwa sababu yeye ni mganga tangu zamani na sasa anasema ameoteshwa dawa hiyo na watu wengi kila siku wanakwenda kwake kupewa kikombe, lakini pia hatuwezi kuthibitisha kama
inatibu magonjwa hayo, mpaka ipimwe na Mkemia Mkuu wa Serikali,”
alisema mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake mganga huyo akihojiwa na mtandao huu, alisema ameoteshwa dawa hiyo ya kikombe usiku wa kuamkia Mei 11, mwaka huu, ambapo alianza kutoa huduma Mei 12 na kuongeza kuwa dawa hiyo inatibu magonjwa mbalimbali sugu, ukiwemo ugonjwa hatari wa Ukimwi, na kila mgonjwa ulipi sh. 500 tu.
Amesema baada ya kuoteswa alipewa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupewa ramani ya Tanzania na ya Afrika, huku akioneshwa doa jeusi katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
Aliongeza katika ndoto hiyo aliamriwa kumnywesha mgonjwa kikombe kimoja tu tena kwa dakika mbili na si vinginevyo, na pia alioneshwa mti wa dawa hiyo na kikombe atakachokuwa anakitumia, ambapo palipokucha alifuatilia mti huo na kununua kikombe hicho dukani na kuanza kutoa huduma hiyo.
Aidha anabainisha kuwa tangu alipoanza kutoa huduma hiyo amekuwa akipata watu wengi wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na hadi sasa zaidi ya watu 2,000 wamekwishaitumia dawa hiyo.
Mei 29, mwaka huu, Serikali ya kijiji hicho ilimwamuru kuorozesha majina ya watu anaowapa kikombe, ambapo hadi sasa wamefikia zaidi ya 150. Aliongeza kuwa kwa siku amekuwa akipokea wagonjwa kutoka maeneo
mbalimbali ndani na nje ya mkoa huo.