Na Hamoud Said, EANA
MAJAJI wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), sasa watakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kunyambulisha Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki kufuatia uzoefu waliopata toka Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya.
“Hivi sasa tupo katika nafasi nzuri zaidi ya kuelewe maeneo magumu ya itafiaki ya Soko la Pamoja baada ya siku tatu za mafunzo. Tumejifunza uzuri na ubaya wa Soko la Pamoja kutokana na uzoezi wa Umoja wa Ulaya ambao unafanana kwa kila hali na harakati za utekelezaji wa Mkataba wa Soko la Pamoja la kwetu,” Rais wa EACJ, Jaji Harold Nsekela alisema.
Jaji Nsekela alikuwa anatoa maoni yake juu ya mafunzo ya siku tatu waliyopata majaji wa EACJ mjini Zanziabar juu ya utendaji kazi wa Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya katika harakati za kujenga mtangamano wa Umoja wa Ulaya (EU), mpango ambao Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pia inaujenga hivi sasa.
“Katika mpango endelevu wa kuimarisha na kupanua mtangamano wa EAC bila shaka upo uwezekanao wa kuifikisha jumuiya hiyo katika migogoro ikiwa ni pamoja na ya kiuchumi, kifedha, kibiashara, kijamii na kisiasa. Mingi katika migogoro hiyo itahitaji ufumbuzi wa kimahakama,” alidokeza Jaji Nsekela.
Itafaki ya Soko la Pamoja la EAC pamoja na mambo mengine unahusisha kuondoa vikwazo vya watu kutembeleana na kufanyakazi katika nchi wanachama, haki ya makazi katika nchi wanachama na biashara huria ndani ya nchi hizo, ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.
Akifungua mafunzo hayo, mgeni rasmi, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu alisema uwingi wa kazi za EACJ unaongezeka na hivyo mahakama hiyo haina budi kuwa tayari kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza.
“Migogoro itakayotokana na harakati za utekelezaji wa itifaki ya Soko la Pamoja bila shaka itasikilizwa na mahakama hii. Ni wazi kwamba kadiri watu zaidi wanavyoshirikiana katika mtangamano pia uwezekano wa kuingia katika migogoro nao huongezeka,” Jaji Makungu alitahadharisha.
Alisema mafunzo ya mara kwa mara juu ya masuala ya sheria ndiyo njia ya uhakika zaidi ya kuongeza ufanisi wa utendaji wa mahakama katika kanda hiyo ya Afrika Mashariki.
Soko la Pamoja ni hatua ya pili ya utekelezaji ya mtangamano wa EAC ukitanguliwa na Umoja wa Forodha. Hatua ya tatu ni Umoja wa Fedha na kisha kufuatiwa na Shikirikisho la Kisiasa ikiwa ni hatua ya mwisho.