Wake wa marais Afrika watakiwa kuwajengea uwezo wanawake na watoto

Rais wa nchi ya Malawi, Bi. Joyce Banda

Na Mwandishi Maalum, Abuja

WAKE wa Marais wa Afrika wametakiwa kuwajengea uwezo wanawake na watoto wa kike kwa kuhakikisha kuwa wanapata elimu ya kutosha ambayo itawawezesha kushika nafasi za juu katika uongozi na hivyo kupunguza ukatilia wa kijinsia dhidi yao.

Wito huo umetolewa na Rais wa Malawi Joyce Banda wakati akifungua mkutano wa saba wa wake wa marais wa Afrika uliozungumzia masuala ya amani barani Afrika uliofanyika mjini Abuja nchini Nigeria.

Rais Banda alisema kuwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni matokeo ya kukosekana kwa elimu na amani katika nchi, jambo la muhimu ni kuwajengea uwezo wa kielimu na kiuchumi ili waweze kutambua haki zao za msingi.

“Kila mmoja wenu katika nchi yake anafanya kazi ya kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata elimu lakini hiyo pekee haitoshi bali mnatakiwa kuweka nguvu zaidi katika kuimarisha amani ndani ya nchi zenu kwani bila nchi kuwa na amani ukatili wa kijinsia utazidi kuendelea”, alisema Banda.

Rais Banda aliendelea kusema kuwa wanawake wapewe nafasi katika usuluhishi na utatuzi wa migogoro wasiachwe wanaume peke yao kufanya kazi hiyo kwani nchi ikikosa amani waathirika wakuu ni wanawake na watoto ambao wengi wao wanauawa na wengine wanafanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa.

Kwa upande wake Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan alisema kuwa nchi za Afrika lazima zifanye jitihada kubwa za kuondoa vikwazo ambavyo vinawazuia wanawake na watoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zao. Wanawake wanatakiwa kutobaguliwa bali kupewa fursa sawa ya kushiriki katika elimu, siasa na uchumi.

Aliendelea kusema kuwa usawa wa kijinsia unatakiwa kuwepo barani Afrika kwa kuunga mkono na kutengeneza mazingira ya kuwainua wanawake kiuchumi na kuhakikisha kuwa wanawake hao wanaishi mazingira salama. Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa na wake wa marais kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.