Na Mwandishi wetu
Musoma,
MWANAMUME mmoja mkazi wa kijiji cha Nyegina Wilaya ya Musoma Vijijini Maingu Masatu (31) anayejishughulisha na shughuli za uvuvi, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma kwa tuhuma za kujeruhi na kumng’ata sikio la kushoto Juliana Pachanga na kumsababishia majeraha mwilini.
Imedaiwa mbele ya Mahakama hiyo na mwendesha mashitaka wa Polisi Alon Mihayo, mnamo tarehe Mei 8 mwaka huu majira ya saa 12 jioni katika kijiji cha Nyegina akiwa na Mariamu Tungaraza na kumuita Juliana Pachanga kwa lengo la kutaka kumuuliza jambo ghafla walianza kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumng’ata sikio.
Imeelezwa katika Mahakama hiyo baada ya kupigwa mlalamikaji alipata nafasi ya kukimbia na kwenda kulipoti katika kituo cha Polisi Kigera na kupewa Pf3 kwa ajili ya matibabu na kwenda kutibiwa hospitalini.
Mahakama hiyo imembiwa kuwa Mtuhumiwa wa tukio hilo alikamatwa siku hiyo ya tukio na kufikishwa katika kituo kikuu cha Polisi Mjini Musoma na kuhojiwa kutokana na mashitaka yanayomkabili na kisha kufikishwa Mahakamani.
Mtuhumiwa wa kosa hilo licha kupewa nafasi ya dhamana na Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo Baraka Maganga alishindwa kukamilisha masharti ya dhamana na kurudishwa mahabusu hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Agosti 7.