Na Nicodemus Ikonko, EANA
NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Dk. Julius Rotich amesema Jumuiya hiyo ingependa kuona Mkataba wa Biashara ya Silaha (ATT) utakaoweza kudhibiti usafirishaji haramu wa silaha.
“Nchi za EAC zingependa kuona mkataba wa ATT (Mkataba wa Kudhibiti Silaha) ambao utashughulikia matatizo ya usafirishaji wa sialaha haramu katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na garantii ya kutosha ya kuheshimu utaifa, mipaka ya nchi na technolojia inayohusiana na nayo,” alisisitiza.
Dk. Rotich alitoa tamko hilo katika hotuba yake kwenye mkutano wa maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa (UN) juu ya mkataba wa ATT mjini New York, mwishoni mwa wiki iliyopita, na nakala yake kupatikana kwa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).
Alifafanua kwamba uzoefu uliopata kanda ya EAC na unaendelea kupatikana unaonyesha maafa makubwa yanayotokana na usafirishaji haramu wa silaha ambao unatakiwa sasa udhibitiwe kisheria.
Upatikanaji kirahisi wa silaha haramu alisema unasababisha pamoja na mambo mengine watu kutawanyika, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uzalilishaji wa serikali halali zilizochaguliwa na wananchi.
“Uhusiano kati ya usafirishaji wa haramu wa silaha, haki za binadamu na masuala ya kibinadamu ni mambo muhimu ambayo hayana budi kuwemo kwenye Mkataba,” alisisitiza.