Wazazi wapewa somo kuwalinda watoto na ubakaji

Mkurugenzi Mtendaji, Ananilea Nkya

Na Mwandishi Wetu

WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuwa makini na kuhakikisha watoto wao hawatembei ovyo usiku wakati huu wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili kuwaepusha kubakwa. Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watoto wanaobakwa huongezeka mara dufu nyakati za mfungo wa Ramadhani.

Ashura Mpatani, Ofisa wa kituo cha Mkono kwa Mkono (One Stop Centre) kinachoshughulikia wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ukiwepo ubakaji katika hospitali ya Mnazimmoja Zanzibar, amesema wastani wa kesi sita za kubakwa watoto huripotiwa katika kituo hicho kila siku wakati wa mfungo wa Ramadhani ikilinganishwa na wastani wa watoto watatu wanaobakwa miezi mingine.

Mpatani ametaja mambo yanayochangia ubakaji kwa watoto kuongezeka wakati wa Ramadhani kuwa ni pamoja na wazazi kuacha watoto kutembea wenyewe kwa muda mrefu usiku hivyo watu waovu kutumia mwanya huo kuwabaka.

Amesema kibaya zaidi wazazi na walezi huchelewa kugundua kuwa watoto wao wamebakwa na hivyo kuwaweka watoto hao katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ikiwa ni pamoja na virusi vya UKIMWI.

Aidha amesema vitendo hivyo vya ubakaji vinaongezeka kutokana na watu wanaofanya vitendo hivyo kutochukuliwa hatua za kisheria kwa sababu mbalimbali. Ametaja sababu mojawapo kuwa ni kukosekana kwa ushahidi kwa vile wanaobakwa hupoteza ushahidi bila kujua.

Madaktari wanasema mtu akibakwa kamwe asioge wala kunawa na anapaswa kwenda polisi kuandika maelezo na kuchukua PF3 kisha kwenda hospitali kupimwa ili kutunza ushahidi na kupata dawa na kuzuia madhara ikiwa ni pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Utafiti uliofanywa na TAMWA Zanzibar mwezi Aprili mwaka huu umeonyesha kuwa mwaka 2011 kesi zipatazo 400 za ubakaji ziliripotiwa visiwani humo. Utafiti huo ulibaini kwamba sababu za watoto wengi kubakwa ni pamoja na wazee (wazazi na walezi) kutofuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao.