Na Joachim Mushi, wa dev.kisakuzi.com
MAMA wa mwanafunzi Mwenjuma Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni na kushindwa kujiunga na shule hiyo kutokana na familia hiyo kutelekezwa na baba amefariki dunia.
Mama huyo Hadija Magalu amefariki dunia juzi ikiwa ni muda mfupi baada ya kujifungulia nyumbani kwake hali iliyomfanya apoteze damu nyingi hatimaye kuzidiwa na kufariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtoto wa mama huyu (Mwenjuma Magalu) amezitoa kwa mwandishi wa habari hizi, alisema mama yake alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua pamoja na kichanga chake wakati ndugu na jamaa walipokuwa wakifanya taratibu za kumpeleka hospitalini kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Marehemu Hadija Magalu mkazi wa Kijiji cha Msasa ndiye aliyekuwa akiwalea wanae watatu akiwemo Mwenjuma Magalu, baada ya baba wa watoto hao kuwatelekeza, kitendo ambacho kilimfanya mama huyo kushindwa kumudu baadhi ya mahitaji ya familia ikiwemo gharama za masomo ya sekondari.
Mapema Desemba 12, 2011 marehemu alishindwa kumlipia mwanae, Mwenjuma Magalu gharama za masomo (sh. 72,000) hali iliyomfanya mtoto huyo kukata tamaa ya kuendelea na shule kabla ya kuanza kufanya vibarua kwa moja ya kampuni za Kichina zinazojenga barabara inayopita Kijiji cha Msasa.
Hata hivyo licha ya familia hiyo kukumbwa na msiba huu mzito, faraja iliyopo kwa sasa ni kitendo cha kujitokeza kwa wasamaria ambao wameahidi kumsomesha mwanafunzi Mwenjuma Magalu hadi hapo atakapo maliza elimu ya kidato cha nne.
Tayari mwanafunzi huyo amerudi shuleni na kuanza masomo baada ya wafadhili kuanza kumgharamia masomo yake ya sekondari katika shule ya Sekondari Komnyanganyo.
*Habari hii imeandaliwa na mtandao wa dev.kisakuzi.com (www.thehabari.com)