Na Mwandishi Wetu
IDADI ya maiti zilizopatikana hadi sasa katika ajali ya meli ya Mv. Sky Get iliyozama jana mchana eneo la Chumbe nje kidogo ya Zanzibar imefikia 31. Taarifa ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba idadi kubwa ya majeruhi walionuzurika na ajali hiyo imeletwa katika Bandari ya Malindi Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) tayari imetangaza siku tatu za maombolezo kwa ajili ya kuwakumbuka ndugu na jamaa waliokubwa na ajali hiyo mbaya ikiwa ni ya pili kutokea majini Zanzibar. Mapema jana Bunge la Tanzania lilihairisha shughuli zake jana ili kutoa nafasi kwa wabunge na viongozi husika kuungana kwa pamoja kufuatilia tukio hilo.
“Ndugu wabunge hoja ya kuahirisha shughuli za bunge leo (jana) imetolewa na imeungwa mkono…sasa nahairisha shughuli za bunge hadi kesho ili kutoa nafasi kwa viongozi husika kufuatilia kwa karibu suala hili,” alisema Spika wa Bunge Anne Makinda baada ya kutolewa hoja hiyo na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi akiomba kuondoa hoja yake mezani ya kujadiliwa kwa hotuba ya wizara yake.
Meli ya Mv. Sky Get inayomilikiwa na Kapuni ya Seagal ilipinduka jana ikiwa safarini kutokea Dar es Salaam kuelekea Unguja baada ya hali ya hewa baharini kuchafuka na kuzama ghafla. Mtandao huu utaendelea kuwaletea taarifa zaidi za hali ya uokoaji kadri zinavyotufikia.