Na Janeth Mushi, Arusha
WATU wanne (4) wakiwemo wanafunzi watatu wamepoteza maisha huku wengine 11 wakinusurika kifo katika ajali iliyohusisha pikipiki namba T 992 BPB aina ya Toyota na gari la abiria aina ya Toyota Hiace.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha Akili Mpwapwa,alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi Mei2 mwaka huu majira ya saa 2usiku katika eneo la Mto wa Mbu wilayani Monduli.
Mpwapwa alisema kuwa katika ajali hiyo wanafunzi watatu wakiwemo mapacha wawili waliokwua wamepanda kwenye pikipiki moja,ghafla gari lililokuwa na namba za usajili T401 BCY lililokuwa likiendeshwa na Godfrey Leonard(24) liligongana uso wka uso na pikipiki hiyo na kusababisha vifo papo hapo.
Alidai kuwa chanzo cha ajali hiyo ni gari la abiria lililokuwa likitokea Arusha likielekea Mto wa Mbu,ambapo dereva wa gari hilo alilipita gari lingine la abiria aina ya Noah lililokuwa likitokea Karatu na ghafla lilikutana na pikipiki hiyo iliyokuwa ikitokea Mto wa Mbu na kugongana uso kwa uso.
Kamanda aliwataja watu hao kuwa ni Godfey Leonard(24) aliyekuwa dereva wa gari hilo,Sibiteti Kimiti(22) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Manyara(ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo).
Wengine ni Reuben Kimiti(22) mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Manyara na Kitailei Namungu(19) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Rift Valley wote wakiwa ni wakazi wa eneo la Lotirwa.
Aliwataja walionusurika katika ajali hiyo kuwa ni Ibrahim Thomas(28) Mto wa Mbu,Salma Kefu(25) Mto wa Mbu,Barnabas Simon(28) Babati,Shaban Muruma(31) Arusha,William Naibara(36) Lake Natron na Schola Nicholaus(45) Lotirwa.
Alisema majeruhi hao wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Monduli kwa matibabu huku wengine watano(5) wakiwa wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu.
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
WATU zaidi ya 60 wamenusulika kufa na mmoja kati yao kujeruhiwa wakati akijaribu kuruka baada ya basi la kampuni AM Coach namba T 487 BDW lililokuwa linatoka Mwanza kwenda Mji wa Muganza kupasuka gurudumu la mbele kisha kupata hitilafu katika mfumo wa umeme kabla ya kuteketea kwa moto.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 12;30 jioni wakati likiegesha kwenye Kituo cha Mabasi cha mjini Chato mkoani Kagera, ambapo inasadikiwa gari hilo lilikuwa na hitilafu huku dreva akiliendesha na kufukuzana na basi la kampuni ya Bunda lililo kuwa linaelekea Bukoba.
Kutokana na ajali hiyo mamia ya wananchi wa Mji wa Chato walifulika katika kituo cha mabasi kushuhudia ajali hiyo na wengine wakijaribu kuzima moto kwa mchanga bila mafanikio huku Jeshi la Polisi wilayani humo likiwadhibiti wananchi waliokuwa wakishusha mizigo ndani ya gari hilo wakati likiteketea kwa moto kutokana na wilaya ya chato kutokuwa na gari la kuzimia moto.
Baadhi ya abiria walionusulika kifo katika basi hilo Timotheo Ludomya na Susana Kadri mkazi wa Muganza licha ya kuokoa maisha yao wamelalamikia upotevu wa mali zao zilizokuwa ndani ya basi hilo kwa madai walikuwa wakitoka kununua bidhaa mbalimbali za maduka yao na kutaka kujua hatma ya mali zao.
“Licha ya kwamba roho zetu zimesalimika bado tunasikitishwa na mali zetu, kama baadhi yetu tulikuwa na mizigo ya kwenye maduka ambayo tumetoka mwanza kuhemea na hatujui kama tutalipwa bidhaa zetu au la kwa maana hata familia zetu zinategemea uchumi unaotokana na bidhaa hizo”alisema kadri kwa uchungu.
Hata hivyo baadhi yao wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wamiliki wa magari ya abiria watakao bainika kutembeza magari mabovu na kuajili madreva wasi na ujuzi wa kutosha ili kunusuru maisha ya watu ambao wamekuwa wakipoteza maisha kila siku kutokana na ajali za barabarani.
Mkuu wa polisi wilaya ya Chato Yahaya Rajabu akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili amekiri kutokea kwa ajali hiyo na kwamba hakuna mtu aliyepoteza maisha katika tukio hilo baada ya wananchi kutelemka haraka muda mchache baada ya basi hilo kuanza kufuka moshi kabla ya kuteketea kwa moto.
Amesema thamani ya uharibifu wa mali na za abiria na basi hilo hazijafahamika na kwamba jeshi lake linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na kuitaka jamii kushirikiana na jeshi la polisi pindi wanapohisi vyombo wananvyosafiria havina usalama wa kutoka kabla ya kutokea kwa ajali.
Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa hawatoi taarifa kwa jeshi la polisi kutokana na ukiukwaji wa sheria za barabarani ikiwemo mwendo kasi wa madreva pindi wanapokuwa safarini hatua ambayo imekuwa ikikwamisha jitihada za udhibiti wa ajali barabarani.
Ajali hii ambayo imenusuru maisha ya zaidi wa watu 60 wilayani chato imetokea huku watanzania wakiwa hawajasahau donda kubwa la kupoteza maisha ya watu 16 na wengine 67 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha mabasi mawili ya kampuni ya Sheraton na Bunda basi pamoja na lori aina ya Fuso katika kijiji cha Chibingo wilayani Geita Mkoani Mwanza.