Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa
RAIS Jakaya Kikwete wa Tanzania amekuwa miongoni mwa Marais na viongozi wakuu wa Serikali mbalimbali za Afrika waliohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi zinazoshiriki katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM)
Rais Kikwete aliungana na marais wengine akiwemo Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Melesi Zenawi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulijadili taarifa ya utekeleza wa hali ya utawala bora kwa nchi za Uganda, Burkina Faso na Algeria. Rais Abdulaziz Bouteflika wa Algeria aliwakilishwa na Waziri Mkuu wan chi hiyo, Ahmed Ouyahia.
Akizungumza mjini Addis mara baada ya mkutano huo wa marais, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib alisema mkutano huo ulikuwa wa mafanikio na viongozi hao walipitisha maazimio mengi ikiwemo kuiimarisha APRM ili kuwa taasisi kamili ya Umoja wa Afrika.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 32 za Afrika zinazoshiriki katika mchakato wa APRM unaolenga kuzipa fursa nchi za Afrika kujitathmini Kiutawala Bora kwa kuwapa nafasi wananchi wao na wataalamu wao wa ndani kutoa maoni yao. Mchakato huu ni endelevu na hurudiwa kila baada ya miaka minne.
Taarifa kutoka mjini Addis zinaonesha kuwa nchi nyingine tano zimetangaza kujiunga na taasisi ya APRM kupitia mkutano huo uliofanyika jana (Jumamosi Julai 14, 2012).