Na Mwandishi Wetu, Mpanda
KATIBU wa Itikadi na Uenezi Taifa (CCM), Nape Nnauye amedai kunasa barua za Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na wakili maarufu nchini Mabere Marando akikana kuwaambia Watanzania kuwa naye alifaidika na fedha za Mfuko wa Madeni ya Nje (EPA).
Amesema kutokana na kuupata ushahidi wa nyaraka hizo, anamtaka Marando kuchagua kufanya siasa au kuendelea na kazi yake ya uwakili kwa kuwa kuendelea na vyote kutamgharimu.
Nape aliyasema hayo jana kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika mjini hapa mkoani Rukwa na kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wa nji huo na vitongoji vyake.
“Kimsingi namheshimu sana Marando lakini kitendo cha kuchanganya uwakili na siasa karibuni kitamgarimu, hasa siasa za majitaka za CHADEMA,” alisema Nape huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliofurika kwenye mkutano huo.
Nape alisema, hivi karibu alipomtaka Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willbrod Slaa aache unafiki kwa kueleza kwanini analipwa na chama chake sh. milioni 7.5 kwa mwezi bila kukatwa kodi, wakati aliwahi kupinga wabunge kulipwa mshahara usiofikia kiasi hicho kuwa ni kubwa, badala ya kujibu yeye, CHADEMA ilimtumia Marando kutoa shutuma kuwa Nape naye ni miongoni mwa waliofaidika na fedha za EPA, hivyo ni fisadi.
Katika madai hayo Marando alidai Nape alipewa fedha hizo za wizi na mfanyabiashara Jayantkumar Patel ambaye kwa mujibu wa maelezo aliyokaririwa Marando na baadhi ya vyombo vya habari alidai Patel alimtaja Nape kwenye tume ya rais ya iliyokuwa inashughulikia swala la EPA.
“Nilishituka kusikia yale maneno yakisemwa na mtu ninayemheshimu, nikajua ndio matatizo ya kuchanganya siasa na uwakili, siasa zenyewe za CHADEMA. Lakini cha ajabu baada ya siku chache Marando amemwandikia Jeetu Patel akikanusha taarifa ile na kuisukumia CHADEMA,” alisema Nape na kuongeza; “Nadhani ni muhimu Marando akachagua sasa kufanya siasa au kuendelea na kazi yake ya uwakili kabla aibu kubwa haijamkuta”.
Nape alisema anazo barua za mawasiliano kati ya Jeetu Patel na Marando zinazoonesha Marando akikataa katakata kuhusika na kauli iliyonukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba Nape alinufaika na fedha za EPA.
Kwa mujibu wa Nape barua ya Jeetu Patel ya Mei 16, 2011 kwenda kwa Marando ikimtaka aeleze kwanini alimhusisha Nape na fedha za EPA huku akijua si kweli, huku barua nyingine ikiwa ya Marando ya tarehe hiyo hiyo, kwenda kwa Jeetu Patel akajitetea kwamba aliwashauri CHADEMA wasimshutumu Nape kwa EPA bila mafanikio, naye akaamua kuuaminisha uma jambo asiloliamini.
“Wananchi yapo mengi kama hili ambayo viongozi wa CHADEMA huwadanyeni kupitia kwenye mikutano au vyombo vya habari, lakini kwa kutojua baadhi yenu huwa mnawaami . Kitendo hiki kinamfanya Marando na chama chake wasiaminike kwa umma.
Nape alisema, bila aibu Marando anamkana Antoni Komu na Chama chake cha CHADEMA kuwa hakuunga mkono shutuma hizo dhidi ya Nape huku akijua wazi kuwa CHADEMA ilibidi wamtumie Marando kuwaeleza watanzania jambo ambalo hata yeye haliamini na kwamba kwa kufanya hivyo kwakuwa Marando ni wakili wa baadhi ya watuhumiwa wa kesi za EPA Watanzania wataamini kwa haraka.
“Je wananchi tuendelee kumwamini Marando na chama chake?” Nape alihoji umati wa wananchi kwenye mkutano huo wakajibu “hawaaminiki hao”.
Nape alisema kutokana na kukana alichosema, sasa asimame na kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwadangaya kuhusu tuhuma hizo. “Sasa namshauri kwanza atoke kuwaomba radhi watanzania kwa kuwadanganya katika hili na mengine mengi aliyotumiwa na CHADEMA kusema bila kuyaamini kama alivyofanya kwa hilo.
Nape alisema Marando aspoomba radhi Watanzania ataitoa hadharani barua husika ili Watanzania waisome waone unafiki wa Chadema na viongozi wake.
Kuhusu madai ya Chadema kwamba nchi haitatawalika, Nape alisema wanaodai nchi haitawaliki hawana mapenzi wala uchungu na nchi hii, ndo maana kwao hata nchi ikichafuka si tatizo ili mradi wanapata wanachotaka.
Aliwatahadharisha Watanzania kutohangaika na baba wa kambo wakati baba mzazi yupo. Akimaanisha vyama vya upizani ni baba wa kambo na CCM ndio baba mzazi.
Alisema mabadiliko makubwa yanayoendelea ndani ya CCM ndio matarajio ya watanzania kwa kuwa CCM inafahamu kuwa wasipoyapata watayatafuta nje na hapo CCM itakuwa imepoteza haki ya kuongoza nchi, hivyo ni muhimu wana CCM wakawapatia watanzania mabadiliko wanayoyataka.
Katika hatua nyngine baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, wamedai kwamba haijawahi kutokea mkutano wowote uliofanyika katika miaka ya karibuni mjini Mpanda kupata watu wengi kiasi cha waliohudhuria jana mkutano wa Nape.
“Chadema pia waliwahi kuja hapa juzi juzi, lakini kwa kweli umati huu wa aleo umevunja rekodi, wale hawakupata watu kama hawa” alisema mkazi mmoja wa mji huo, Samel Msakazi.
Naye Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Nchemba Mwigulu akizungumza kwenye mkutano huo aliwataka watanzania kutokubali kugawanywa na wanasiasa uchwara wanaotaka kuwatumia kwa malengo yao binafsi,bali waendelee kuienzi amani nchini ambayo imejengwa kwa muda mrefu. Wajumbe hao wa sekretarite mpya ya CCM watamalizia ziara yao ya siku nne mkoani Rukwa leo asubuhi.