WATU sita wote wakazi wa Kigogo Mbuyuni jijini Dar es Salaam wamefariki dunia baada ya kunywa pombe aina ya gongo, inayodhaniwa imechanganywa na spiriti ili kuifanya iwe kali zaidi, lakini badala yake imekuwa sumu.
Watu hao ambao watatu ni kutoka familia moja walianza kufariki dunia tangu usiku wa kuamkia juzi kwa nyakati tofauti ikiwa ni saa kadhaa baada ya kunywa kinywaji hicho na sasa wengine watatu ambao nao walikunywa pombe hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Amana wakiendelea na matibabu.
Hadi kufikia jana jumla ya watu watano walikuwa wamefariki dunia huku baadhi wakiwa kwenye matibabu hospitalini Amana jijini Dar es Salaam. Taarifa ambazo mtandao huu umezipata leo pia amefariki mgonjwa mwingine hivyo kufanya waliokufa kufikia sita. Aliyefariki leo ndiye anayedaiwa kuwa muuzaji wa pombe hiyo Immakulata au Imma.
Taarifa ambazo mtandao wa dev.kisakuzi.com ulizipata tangu jana kutoka kwa mmoja wa majirani zinasema watu hao walianza kulalamika maumivu ya tumbo baada ya kunywa gongo hiyo, huku wakiharisha na kutapika kabla ya kufariki dunia mmoja mmoja kadri walivyokuwa wakipelekwa kupata matibabu.
Waliofariki hadi sasa ni pamoja na vijana watatu wakiwemo Halid na Banzi (jina la kijana wa tatu halikupatikana mara moja), wazee wawili yaani mzee Juma na Upara.
Hata hivyo leo asubuhi wamepelekwa tena hospitalini wagonjwa wengine wawili ambao nao walikunywa pombe hiyo wakiwa na hali mbaya. Hadi jana kijana aliyetambulika kwa jina la Mohamed na dada aliyetambuliwa kwa jina la Mama Steven walikuwa bado wamelazwa. Baadhi ya majirani wamesema taarifa za awali katika nyumba hiyo zinadai pombe waliokunywa (gongo) ilikuwa imechanganywa na spiriti ili kuifanya iwe kali.
Taarifa zaidi kutoka eneo hilo zinasema nyumba ya familia ambayo ndiyo inadaiwa kuuza pombe hiyo ndiyo iliyoathirika zaidi kwani hadi sasa imepoteza wanafamilia watatu huku wawili akiwemo muuzaji wakiendelea na matibabu.
“Hadi sasa tuna maiti tatu ambazo hazijazikwa kutoka mtaa mmoja (Kigogo Mbuyuni karibu na Shule ya Msingi Rutihinda) hapa tunaomba Mungu wasiendelee kufa maana itakuwa kiama hapa mtaani kwetu,” alisema jirani mmoja ambaye hakupenda kutajwa mtandaoni.
Taarifa zaidi zimebainisha bado kuna baadhi ya watu ambao walikunywa pombe hiyo na wanaendelea kupata matibabu nyumbani huku wakihofia kwenda hospitalini kwani wanadai huenda wakakamatwa kwa unywaji wa pombe hiyo haramu.