dev.kisakuzi.com, Moshi
VIJANA wametakiwa kuacha kushabikia mambo ambayo hayana masingi kama vile migomo na maandamano, na badala yake kila mmoja afanye kazi kwa bidii kwa kuzingatia maadili, ikiwa ni pamoja na kuepuka ulevi na ngono zembe.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Mwika Dk. Godfrey Malisa, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa juma la vijana katika usharika wa Moshi pasua uliopo manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Dk. Malisa alisema ni vema vijana wakajifunza kufanya kazi kwa akili na maarifa na kuepuka kudai haki kwa kufanya maandamano au migomo kwani kufanya hivyo ni kinyume cha maadili na utaratibu wa kutafuta haki.
“Katika dunia leo inasikitisha sana kwani watu wameona njia ya kudai haki zao ni kufanya maandamano na kuanzisha migomo ambayo imekuwa ikiwakandamiza sana wanyonge, na cha kusikitisha zaidi ni kwamba vijana ndio wahanga wakubwa wa kujiingiza katika vitendo hivyo vya migomo na maandamano kwa madai kuwa wanadai haki zao,” alisema Dk. Malisa.
Katika hatua nyingine Dk. Malisa aliwataka vijana kubadilika na kuacha vitendo viovu ikiwemo madawa ya kulevya, ulevi na ngono zembe na kujishughulisha na kazi mbalimbali za kimaendeleo hatua ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi katika jamii.
Aidha alisema kumekuwepo na kundi kubwa la vijana ambao wamekuwa hawafanyi kazi na badala yake hushinda vijiweni huku wakijihusiaha na vitendo vya utumiaji wa madawa ya kulevya na ulevi wa pombe wa kupindukia hali ambayo ni hatari sana kwa ustawi wa taifa.
“Jamani vijana wangu naomba mbadilike, kwani mkiendelea na vitendo vyenu hivi viovu na vichafu katika jamii, nawahakikishia kuwa miaka michache ijayo hatutakuwa na taifa, vijana ndio taifa la leo, jirekebisheni kulijenga taifa katika msingi imara,” alisema.
Awali akizungumza Mchungaji wa Usharika wa Moshi Pasua, Elirehema Silaa aliwataka watanzania kuomba kwa ajili ya nchi ili Mungu aweze kuiepusha na mambo mabaya ikiwemo migomo na vurugu ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa katika nchi.
Wakizungumza baadhi ya vijana waliohudhuria uzinduzi huo walikiri vijana kujiingiza katika vitendo viovu na kusema kuwa hali hiyo inatokana na baadhi ya wazazi kubweteka katika malezi na hivyo kuwaacha watoto kufanya mambo kama wanavyotaka.
Walisema kumekuwepo na wazazi ambao wameporomoka kimaadili na wengine wamekuwa wakishindwa kujiheshimu hata kwa watoto wao hali ambayo inachangia na watoto kukua katika maadili yasiyofaa hivyo kujikuta wakitumbukia katika vitendo viovu.