RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akaya Mrisho Kikwete aliondoka nchini Jumanne, Julai 10, 2012 kwenda London, Uingereza kushiriki mkutano wa kimataifa wa viongozi kujadili Uzazi wa Mpango kwa nchi masikini zaidi duniani.
Rais Kikwete ni miongoni mwa wakuu wa nchi tatu kutoka Afrika walioalikwa kushiriki katika mkutano huo wa siku moja ulioitishwa na kudhaminiwa na Serikali ya Uingereza, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) na Taasisi ya Bill and Belinda Gates Foundation.
Mbali na Rais kikwete, viongozi wengine wa Afrika walioalikwa kwenye mkutano huo ambao pia utahudhuriwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Mkutano huo utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Queen Elizabeth ni wa kwanza wa aina yake duniani na utaanzisha Mchakato wa Dunia ambao utalenga kuwawezesha wanawake wapatao milioni 120 katika nchi masikini zaidi duniani kupata habari, huduma na mahitaji ya kupanga uzazi bora zaidi na kuokoa maisha yao ifikapo mwaka 2020.
Aidha, mkutano huo ni nafasi ya pamoja ya kuiwezesha jumuia ya kimataifa kuonyesha dhamira zaidi katika huduma za uzazi bora ambazo kwa kiasi fulani zitachangia kuongeza kasi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia nambari nne (kupunguza vifo vya watoto) na nambari tano (kuboresha afya za akinamama).
Vile vile mkutano huo ni nafasi ya jumuia ya kimataifa kuonyesha dhamira zaidi katika kuboresha sera za uzazi bora na kupata michango zaidi ya raslimali kutoka kwa nchi zinazoendelea, wafadhili, sekta binafsi na jumuia za kiraia kwa nia ya kuboresha shughuli hizo.
Inakadiriwa kuwa zitahitaji kiasi cha dola za Marekani bilioni 10 kwa miaka minane ijayo kuanzia sasa 2012 hadi 2020 ili kudumisha huduma za sasa za uzazi bora duniani. Kiasi cha dola bilioni nne za ziada zitahitaji ili kuweza kuwafikisha wanawake milioni 120 katika nchi masikini zaidi ambao kwa sasa hawapati huduma hizo katika miaka hiyo minane ijayo.