Mwandishi Wetu, Moshi
HALI ya usafiri katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro bado inaendelea kuwa mbaya baada ya madereva wa magari madogo na baadhi ya magari makubwa kufanya mgomo wakipinga ongezeko la ushuru kutoka Sh. 1,000 hadi 1,500 kwa magari madogo na Sh. 2,000 kwa magari makubwa.
Mbali na madereva hao kuendeleza mgomo Jeshi la polisi mkoani hapa linawashikilia watu 18 kwa tuhuma za kuhusika na vurugu katika mgomo wa madereva unaoendelea katika manispaa ya Moshi, hali ambayo imesababisha watu watatu kujeruhiwa na magari mawili kuharibiwa kwa kupasuliwa viyoo.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita alisema watu hao walikamatwa majira ya saa nne asubuhi baada ya kukutwa wakishabikia mgomo na kuanzisha vurugu.
Kwa mujibu wa Kamanda Moita waliokamatwa ni vijana wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 20 waliingia barabarani na kufanya fujo hali ambayo ilililazimu polisi kuanzisha msako na kuwakamata ili kuimarisha hali ya usalama.
“Jana julay sita (Juzi) majira ya saa nne asubuhi kulikuwa na mgogoro wa magari yanayofanmya safari zake maeneo anuai ya Mkoa wa Kilimanjaro, sababu za mgogoro huo ni kupinga ongezeko la ushuru kutoka sh. 1000 hadi 1,500 kwa magari madogo na sh. 2,000 kwa magari makubwa, zinazotozwa katika stendi kubwa ya mabasi mjini Moshi,” alisema kamanda Moita.
Alisema katika mgomo huo kulikuwa na vijana ambao walikuwa wakishabikia mgomo na kusababisha vurugu, ambapo walikuwa wakiwapiga madereva waliokubali kulipa ushuru huo na kuwarushia mawe hali ambayo ilisababisha kuwepo kwa fujo kubwa katika maeneo ya stendi kubwa ya mabasi manispaa ya Moshi.
Alisema bado askari polisi wanaendelea na msako na kufanya doria kuimarisha ulinzi kutokana na kwamba hali haijawa shwari na haujapatikana muafaka baina ya manispaa na madereva hao. Kaimu Kamanda alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya mahojiano kukamilika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Vuguvugu hilo la mgomo ambalo lilianza toka jun 20 mwaka huu limesababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri na kuwalazimu kukodi pikipiki maarufu kama bodaboda na teksi hali ambayo imewawia vigumu wananchi wa kipato cha chini na kuwafanya kutanda kandokando ya barabara huku wakiwa hawajui cha kufanya.
Hali hiyo ya mgomo ambao ulianza toka Julai 6 majira ya asubuhi umesababisha kuwepo kwa usumbufu mkubwa ambapo bado madereva hao hawajakubali kulipa ushuru huo ambao umeshapitishwa rasmi kuwa sheria.
Wakizungumza baadhi ya wasafirishaji katika manispaa ya Moshi walisema kiwango ambacho kimepangwa na halmashauri hiyo cha sh. 1,500 kwa magari madogo na Sh. 2,000 kwa magari makubwa ni kikubwa sana na kwamba hawakushirikishwa katika mchakato wa upandishaji ushuru huo hivyo hawako tayari kukilipa.
Aidha waliongeza kuwa endapo Manispaa ya Moshi haitasikia kilio chao nakushusha ushuru wako tayari kuegesha magari yao nyumbani Kwa madai kuwa hali ya maisha imepanda hivyo hawawezi kulipa Sh. 1,500 kwa siku ambayo ni sh. 540,000 kwa mwaka ili hali bado wao wanaishi katika mazingira magumu.
Pamoja na mgomo huo kuendelea na wananchi kupata shida ya usafiri bado haujaweza kupatikana muafaka kuhusiana na ushuru huo kutokana na kwamba ombi lililotolewa na kaimu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Ibrahim Msengi la kurefushwa kwa muda wa utekelezaji wa sheria hiyo ya kupanda kwa ushuru ambayo ilianzwa kutekelezwa toka julai mosi ili kutoa nafasi ya majadiliano bado halijajibiwa.
“Ushuru huu umepitia mchakato wote hadi kufikia kusainiwa na Waziri mkuu, baadhi ya wasafirishaji hawakukubaliana na kiwango hiki cha ushuru, na kufanya mgomo, kwa kuwa hii ni sheria hatuna mamlaka ya kuibadili,kama kuna malalamiko mchakato uleule ufuatwe kwa kuwa hii sasa ni sheria,lakini tumeomba muda wa utekelezaji sheria hii urefushwe,” alisema Msengi.
Licha serikali kuwataka madereva kuendelea kufanya kazi kusubiri maombi yaliyotumwa kwa mamlaka husika kujibiwa bado madereva hao hawakukubali kufanya kazi na badala yake wameendeleza mgomo wao huku baadhi yao ambao wameanza kufanya kazi wakifanya pasipo kulipa ushuru.
Kutokana na ushuru huo Halmashauri ya Manispaa ya Moshi inatarajia kuongeza mapato kutoka Sh. mil. 25 zilizokuwa zikikusanywa kwa mwezi hadi kufikia Sh. mil. 38 hali ambayo imeonekana kuanza kuyumba kutokana na madereva kukwepa kulipa ushuru huo mpya ambao ulitakiwa kuanza kutekelezwa toka Julai Mosi.