Shirika la kutetea haki za binaadam la Amnesty International limeitaka serikali ya Misri kufanya uchunguzi kamili baada ya maofisa wa juu wa kijeshi kukiri kuwa waliwafanyia vipimo vya ubikira, wanawake waliokuwa wakiandamana hivi karibuni.
Pamoja na hayo, Amnesty imetaka wote waliohusika kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu udhalilishaji huo. Tuhuma hizo ambazo zinadaiwa kutokea kwa wanawake waliokuwa wakiandamana baada ya kuondoka madarakani kwa rais Hosni Mubarak zimewashitusha wengi nchini Misri.
Kwa mujibu wa Amnesty International, wanawake 18 walikamatwa, kupata kipigo ikiwa ni pamoja na kupigwa shoti kwa umeme baada ya wanajeshi kuwatawana waandamanaji katika eneo la wazi la Tahrir mapema Machi, 2011.
Wanawake wote hao isipokuwa mmoja tu, walivuliwa nguo, kulazimishwa kupimwa kama bado ni bikira na kutishiwa kushitakiwa kwa makosa ya ukahaba.
Kilichowashangaza wengi hasa ni matamshi ya Jenerali wa kijeshi mwenye cheo cha juu kukiri kuwa vipimo vya ubikira vilifanywa. “Hawa wanawake sio kama mwanao au mwanangu wa kike. Hawa ni wasichana walioweka kambi katika mahema na waandamanaji wa kiume.”
Jenerali huyo ameongeza kusema: “Hatukutaka waje kusema tumewanyanyasa kijinsia au kuwabaka, kwa hiyo tulitaka kuthibitisha kuwa wao sio mabikira.”
Suala hili linaonesha jinsi mvutano unaoendelea kati ya baraza la kijeshi ambalo linatawala Misri na vijana wanaoandamana ambao walisababisha kuondoka kwa Rais Mubarak.