Waisilamu kulinda makanisa Kenya

Majeruhi wa mlipuko nchini Kenya

VIONGOZI wa Kiislamu nchini Kenya wamekubaliana kuunda makundi ya kutoa ulinzi kulinda makanisa kutokana na mashambulizi kama yaliyotokea Kaskazini mwa Kenya siku ya Jumapili.

Watu 15 waliuawa katika mashambulizi mawili dhidi ya makanisa mawili mjini Garissa karibu na mpaka wa Somalia. Eneo la mpakani mwa Kenya na Somalia limekumbwa na hali ya wasiwasi tangu Kenya ilipopeleka majeshi yake kupambana wanamgambo wa Al-Shabab.

Mkuu wa baraza la waisilamu nchini Kenya, Adan Wachu, aliambia BBC kuwa kitendo cha Jumapili kilikuwa cha ugaidi. Waislamu wanahisi kuwa kwa sababu wakristo ni wachache katika sehemu hiyo hakuna budi kuwalinda.

“Kuna watu huko nje wanaotaka kufanya kila wawezalo kufanya Kenya kama Nigeria.” Alisema bwana Wachu, ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la viongozi wa kidini nchini Kenya.”

“Sisi hatutaruhusu kutokea ghasia za kidini nchini humu, yeyote aliye na nia ya kuchochea hali hiyo afahamu kuwa hatafaulu.” aliongeza Wachu.

Alisema kuwa sasa ni juu ya viongozi waisilamu mjini Garissa kupanga namna ambavyo makanisa thelathini yaliyo Garissa yatalindwa. Watu wengi wanaoishi ndani na kando ya mji wa Garissa ni wasomali na ambao ni waisilamu.

Mwezi Oktoba mwaka jana wanajeshi waliingia nchini kupambana dhidi ya al-Shabab wanaotuhumiwa kufanya vitendo kadhaa vya utekaji nyara na kutatanisha usalama kwenye eneo la mpakani.

Lakini tangu hapo Al Shabaab limelaumiwa kwa kufanya msururu wa mashambulizi ya maguruneti katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo. Viongozi wa kundi hilo, hawajajibu shutuma zozote za kufanya mashambulizi ya Garissa.
-BBC