Na Mwandishi wa dev.kisakuzi.com-Moshi
TATIZO la ujangili wa mazao ya misitu katika Hifadhi ya Kilimanjaro (KINAPA) limeelezewa kukwamisha jitihada za Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro na hifadhi hiyo za kulinda na kuhifadhi mazingira.
Kutokana na matukio hayo ya ujangili katika hifadhi hiyo kuendelea kushika kasi takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya majangili 921 wamekamatwa katika kipindi cha mwaka 2009 hadi juni 2012 wakiwa wanajihusisha na uharibifu wa mazao ya misitu ikiwa ni pamoja na ukataji wa miti ya asili kwa matumizi ya fito, kuni, Nguzo, Mbao na uchomaji moto katika misitu ya hifadhi.
Hayo yalibainishwa na mhifadhi wa Hifadhi ya Kilimanjaro KINAPA, Amani Shipella wakati akitoa mada juu ya ulinzi wa rasilimali za asili kwenye kikao cha wadau wa usimamizi wa sheria katika rasilimali za asili iliyohusiha maofisa maliasili, wanyamapori na vyombo vingine vya sheria wakiwemo Polisi na wanasheria.
Shipella alisema tatizo hilo la ujangili limeonekana kushamiri zaidi katika maeneo ya Longido mkoani Arusha, Siha na Hai mkoani Kilimanjaro ambapo wananchi wamekuwa wakiingia ndani ya hifadhi bila kibali na kufanya uharibifu wa mazao ya misitu.
Alisema ili kuweza kumaliza tatizo la ujangili ni vema wasimamizi wote wa sheria wakatoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria za mazingira na rasilimali za asili kikamilifu.
Awali akifungua kikao hicho katibu tawala wa mkoa wa Kilimanjaro Dk. Faisal Issa alisema pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na serikali ya mkoa wa Kilimanjaro bado kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unafanywa na binadamu hali ambayo imesababisha kukauka kwa mazao katika kipindi cha msimu wa kilimo wa Masika kutokana na kukosekana kwa mvua.
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya KINAPA, Erastus Lufungulo alisema lengo la kikao hicho ni kuweka nguvu za pamoja katika kudhibiti tatizo la uharibifu wa mazingira kutokana na kwamba kwa sasa hali ya uharibifu wa mazingira katika hifadhi hiyo bado ni kubwa.
Naye Oscer Ngole mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Kanda ya Moshi ameishauri KINAPA kuweka utaratibu wa kuwashirikisha wananchi wanaozunguka hifadhi katika kulinda na kuhifadhi mazingira ili kuimarisha ujirani mwema.
“Kuna wananchi ambao wamekuwa wakikamatwa katika hifadhi kwa kosa la kukutwa wakikata majani, Kinapa iangalie namna ya kujenga ujirani na watu hawa ili kuhakikisha wanakuwa walinzi wa rasilimali za misitu,” alisema Ngole.