Na Janeth Mushi, Arusha
IKIWA zimepita siku chache tangu makundi mawili ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Arusha kufanya maandamano yaliyokuwa na madai mbalimbali, wenyeviti wa umoja huo kutoka wilaya zote sita mkoani Arusha wamekutana na kutoa kauli nzito.
Katika kauli ya viongozi hao, iliyotolewa jana mjini hapa kwa wanahabari, wamekanusha vikali baadhi ya madai na kulaani matamko yanayodaiwa kuwa waliwatusi, dhalilisha na kuwakejeli baadhi ya viongozi wa CCM na Wajumbe wa NEC.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya wenyeviti wenzake, Mwenyekiti wa UVCCM, Wilaya ya Monduli, Julius Kalanga amesema wanalaani vikali matamko yasiyozingatia kanuni na taratibu alizodai kuwa zina malengo ya kuwadhalilisha, kuwatukana na kuwakejeli viongozi wa chama na wajumbe wa NEC.
Kupitia tamko hilo wenyeviti hao wameuomba ungozi wa CCM taifa kuhakikisha wanadhibiti nidhamu ya wanachama kwa kuzingatia masharti ya uanachama. Wamewakemea pia vijana wanaompinga mwenyekiti wa UVCCM mkoa huo, kuacha kukurupuka kwani hatua za kinidhamu dhidi yao zitachukuliwa.
“Ndugu waandishi wa habari leo tumeona tukutane nanyi ili kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya mambo ndani ya Jumuiya yetu kama wawakilishi wa ngazi za wilaya.
Licha ya kwamba tuna vikao vyetu kikanuni kila baada ya miezi mitatu, lakini kwa hali ilivyo sasa tumeona haja ya kukutana na kusema ili kuthibiti haliya upotoshaji unaoendelea kuenezwa kwa nia ya kuchochea migogoro ndani ya Jumuiya kwa maslahi yao,” anaeleza Kalanga katika taarifa hiyo.
Ingawa sio desturi yetu kutumia vyombo vya habari kuzungumza masuala yanayohusu Jumuiya, lakini tumelazimika kufanya hivi kwani tunachokizungumza kilisemwa ndani ya vyombo vya habari.
Walisema maazimio ya baraza la vijana lililofanyika Longido Machi 28, 2011 ni makubaliano halali ya Jumuiya na si msimamo wa mtu mmoja. Hivyo kutaka viongozi wa mkoa kusimamia utekelezaji, likiwemo la Mrisho Gambo kusimamishwa ujumbe wa Baraza la Wilaya ya Arusha Mjini. Na jambo hili liliisha katika kikao halali cha kanuni za UVCCM.
“Tunalaani vikali matamko yasiyozingatia kanuni na taratibu zenye malengo ya kuwadhalilisha, kuwatukana na kuwakejeli viongozi wetu wa chama na wajumbe wa NEC. Sote tunajua chama ni vikao lakini hivi sasa kila mtu anaamka na lake. Tunawaomba viongozi wa chama ngazi ya taifa kudhibiti nidhamu ya wanachama kulingana na masharti ya uanachama. Mfano, ibara ya 15(2) ya katiba ya CCM inasema kuwa CCM ndiyo chama chenye nguvu, uwezo na kwamba nguvu hizo zinatokana na umoja wa wanachama.”
“Tunasisitiza kuwa ndani ya umoja wetu hakuna mgawanyiko badala yake umoja wetu ni imara na tunafanya kazi zetu kwa juhudi, utashi wetu kwa maslahi ya chama cha mapinduzi na si vinginevyo. Kwa misingi hiyo vijana wanaomtaka M/kiti wa mkoa kujiuzulu ni maoni yao tunawashauri waache mara moja kabla hatua za kinidhamu kuchukuliwa. Sisi tuko nyuma ya M/kiti wetu na tunamuunga mkono daima katika kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya jumuiya na kwa kuzingatia kanuni na taratibu ikiwemo maaazimio ya baraza,” wanasema wenyeviti hao katika taarifa yao.
Hata hivyo, wamedai maandamano na matamko yaliotolewa mkoani Arusha na baadhi ya vijana hao ni hisia zao wala hayakupangwa na viongozi wa UVCCM hivyo kama hoja za vijana hao ni za msingi basi chama kitayazingatia. Pia waliomba hisisa hizo zisitafsiriwe kama hoja za kuigawa Jumuiya na kuchochea vurugu.
Hivi karibuni makundi ya vijana katika Jumuiya hiyo yaliandamana waliwashutumu viongozi watatu yaani; Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz kuwa ni vinara wa tuhuma za mafisadi na kutaka wang’olewe.
Viongozi hao ambao kwa sasa ni maarufu kama ‘mapacha watatu’ baadhi ya makundi ya vijana ya UVCCM, Arusha walitaka pia uongozi wa juu wa CCM (Taifa) kuwahoji wajumbe hao watatu kwenye kamati ya maadili na watimuliwe ili kukinusuru chama hicho na maslahi ya Watanzania.
Waandamanaji pia walimtaka Wwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya kuachia ngazi kwa madai ni kibaraka wa mafisadi, huku wakimtuhumu Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Chatanda kuwa anakivuruga chama hicho.