RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo la ubakaji ambalo limeonyesha kushika kasi mkoani humo.
Dk. Shein aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Chuo cha Amali Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na tatizo hilo kushamiri mkoani humo alikwisha kutoa wito kufanyiwa utafiti suala hilo kwa kumtumia mtaalamu wa elimu ya mambo ya jamii lakini hatua bado hazijachukuliwa.
Hivyo Dk. Shein ametaka baada ya miezi mitatu awe ameshapewa taarifa juu ya tatizo hilo na kueleza kushangazwa na taarifa ya mkoa huo ambayo haikueleza chochote juu ya kadhia hiyo.
Alisema hatua iliyofikiwa ya tatizo hilo si nzuri hivyo kuna kila sababu ya kuwapo ushirikiano wa kutosha katika kulipiga vita suala hilo kwa pamoja.
Dk. Shein aliwataka masheha, madiwani na wazazi nao kushirikiana kulifanyia kazi tatizo hilo.
Alimpongeza Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar kwa kulisimamia kidete tatizo hilo kwa kutoa wazo la Mkono kwa Mkono kuhakikisha kesi zote zinazohusiana na tatizo hilo zinasimamiwa wizarani kwake.
Pia alieleza umuhimu wa kupiga vita Ukimwi katika Mkoa huo hasa katika Wilaya ya Kaskazini B ambako takwimu zinaonyesha maradhi hayo yanashika kasi.