Na Ngusekela David, Tanga
KUBADILISHANA uzoefu ni dhana iliyozoeleka miongoni mwetu na mara nyingi imekua ikitumika katika shule za msingi ambapo wanafunzi wamekuwa wakitembeleana aidha kwa masuala ya michezo au taaluma.
Dhana hii imekua ikitumiwa hata kwa wakulima wetu vijijini, hapa nazungumzia vikundi vya wakulima ambavyo vimekua vikitembeleana ili kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya kilimo. Kikundi cha Kilongo Farmers Association kimekua ni moja ya kivutio kikubwa katika wilaya za Muheza na Korogwe ambapo vikundi mbalimbali vya wilaya hizi vimepata nafasi ya kukitembelea.
Kikundi hiki kilianzishwa rasmi mwaka 1998 kwa lengo la kuunganisha wakulima ili kuwa na sauti moja katika kuuza mazao yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa madalali ambao wameonekana kuwa kikwazo cha biashara ya kilimo.
Wakati wakulima wa vikundi vingine wakijiengua katika vikundi vyao hali katika kikundi cha Kilongo ni tofauti kwani kila aliye nje ya kikundi hiki anataka kuwa mwanachama kwa jinsi kikundi hiki kilivyoonyesha mafanikio sio tu kwa wanachama bali jamii kwa ujumla.
Hivi sasa kikundi kinauza mazao yao kwa pamoja ikiwa ni pamoja na zao la chungwa ambapo chungwa moja katika vijiji vingine ni kati ya sh. 10-18, Kilongo Farmers Association wanauza chungwa moja hadi sh. 40.
Na hii haikutokea hivi hivi tu bali kwa juhudi za wanachama na uongozi makini wa Kikundi hiki kwani kikundi kina ofisi iliyojengwa kwa nguvu za wanachama na misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali,Vile vile kikundi hiki kinamiliki SACCOSS yaani chama cha kuweka na kukopa ambacho kinaweza kumkopesha mwanajamii yeyote hata yule aliye nje ya chama.
Wakibadilishana uzoefu na kikundi cha Mgila Farmers Association Mwenyekiti wa Kikundi cha Kilongo, Keneth Mwamfupe anasema, uhai wa Kikundi chochote kile ni uwezo wa kiuchumi na uongozi bora hivyo amewashauri viongozi wa kikundi cha Mgila kufanya kila liwezekanalo ili kuwa na SACCOSS kwani ndio chachu ya kukua kiuchumi.
“Mkiwa na uongozi thabiti na misingi mizuri ya kiuchumi ni rahisi hata kwa wahisani kutembelea mara kwa mara na hapo ndipo mnapoona fursa nyingine za maendeleo,” anasema Mwamfupe.
Nae mwenyekiti wa Kikundi cha Mgila Farmers Association, Habibu Bakari ameushukuru mradi wa MUVI kwa kuwaunganisha na kikundi cha Kilongo kwani wamejifunza mambo mengi ambayo wanatarajia kuyafanyia kazi ili waweze kusonga mbele.
Kikundi cha Mgila ni miongoni mwa vikundi ambavyo vimedumaa kimaendeleo, kikundi hiki kilianzishwa kikiwa na wanachama sitini na wanne (64) lakini kwa sasa kina wanachama thelathini na wanne (34) tu ikiwa ni upungufu wa wanachama thelathini (30) ambao wamejitoa kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ada ya uanachama inayotolewa kila mwaka.
Mradi wa MUVI una lengo la kuimarisha vikundi ili kuunda umoja wa vikundi vya wakulima katika Wilaya za Muheza na Korogwe ili kuwaongezea wakulima uwezo wa kuweza kufanya maamuzi yao kwa pamoja.