TAARIFA ambazo zimetufikia kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni kwamba madaktari ambao walikuwa wakiendesha mgomo wamerejea kazini na wagonjwa wameanza kupata huduma kama kawaida.
Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa hospitali hiyo, Aminiel Buberwa Aligaesha inaeleza kuwa tathimini iliyofanyika kuanzia asubuhi saa mbili hadi saa 11 jioni Julai 2, inaonesha kuwa madaktari wamerejea kazini.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Aligaesha alisema katika Idara ya Tiba, madaktari bingwa 19 kati ya 21 wamefika kazini huku akibainisha watatu ambao hawakufika wapo likizo.
“…Registrars wote 12 walikuja kazini. Kliniki zote za tiba zimefanyika kama kawaida. Katika Idara ya watoto, yenye Madakatari Bingwa 16, kati yao 14 walikuja kazini wengine wawili wako likizo na Registrar watatu kati ya sita walikuja kazini ambapo watatu wako likizo,” alisema katika taarifa yake ofisa huyo.
Aidha aliongeza kuwa upande wa OPD yenye Registrars saba, sita kati yao walikuja kazini na mmoja yuko likizo. Aidha Madaktari Bingwa wote walikuja kazini.
“Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili yenye Madakatri Bingwa 10, tisa walikuja kazini na mmoja wao yuko masomoni. Upande wa Emergency Medicine, Registrars wote 10 walikuja kazini.”
Akizungumzia kuhusu huduma za upasuaji, wagonjwa wote waliolazwa wodini wameonwa, na baadhi ya kliniki za huduma ya upasuaji zilifanyika. Hata hivyo, upasuaji haukufanyika kwani hakukuwa na orodha ya wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji.
“Kwa ujumla naweza kusema madaktari wote wamerejea kazini,” alisema Aminiel Aligaesha.
Juzi Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete akihutubia taifa alisema Serikali hainauwezo wa kuwalipa madaktari sh. milioni 3.5 kwa daktari anayeanza kazi kama wanavyotaka wao, hivyo kama kuna daktari ambaye haridhiki na kiasi cha sh. 957,700 wanazolipwa sasa kwa daktari anayeanza kazi ni vema aache kazi kiustarabu tofauti na kufanya mgomo.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo katika hotuba yake ya mwezi Juni, huku akisisitiza kwamba kiasi cha mshahara anaolipwa daktari anayeanza kazi kwa sasa ni kikubwa ukilingannisha na watumishi wengine wa Serikali. Alisema Serikali imekuwa ikipandisha maslahi ya madaktari kwa upendeleo kulingana na umuhimu wao, kwani mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa sh. 178,700, kiasi ambacho mwaka 2005/2006 kilipandishwa na kufikia sh. 403,120.