*Asema daktari asiyetaka mshahara uliopo aache kazi kistarabu
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema Serikali hainauwezo wakuwalipa madaktari sh. milioni 3.5 kwa daktari anayeanza kazi kama wanavyotaka wao, hivyo kama kuna daktari ambaye haridhiki na kiasi cha sh. 957,700 wanazolipwa sasa kwa daktari anayeanza kazi ni vema aache kazi kiustarabu tofauti na kufanya mgomo.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo katika hotuba yake ya mwezi Juni, huku akisisitiza kwamba kiasi cha mshahara anaolipwa daktari anayeanza kazi kwa sasa ni kikubwa ukilingannisha na watumishi wengine wa Serikali.
Alisema Serikali imekuwa ikipandisha maslahi ya madaktari kwa upendeleo kulingana na umuhimu wao, kwani mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa sh. 178,700, kiasi ambacho mwaka 2005/2006 kilipandishwa na kufikia sh. 403,120.
Hata hivyo alisema kiasi hicho kiliendelea kupandishwa mwaka hadi mwaka mpaka kufikia sh. 957,700 fedha ambayo inalipwa sasa kwa madaktari wanaoanza.
“Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata sh. 446,100,” alisema Kikwete katika hotuba yake.
Alisema kwa mujibu wa matakwa ya madaktari wao wanaitaka Serikali imlipe sh. milioni 3.5 kwa daktari anayeanza kiasi ambacho Serikali hakiwezi kukimudu kwa sasa.
“Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya sh. 1,100,000 na 1,200,000 kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania sh. 3,500,000,” alisema Rais Kikwete katika hotuba yake.
Alisema katika mazungumzo ya kufikia muafaka yanayoendelea kati ya upande wa madaktari na Serikali upande wa madaktari uliwasilisha madai 12 ambayo ilitaka yashughulikiwe na hadi sasa tayari madai saba yamefanyiwa kazi na Serikali huku akisisitiza kwamba yapo mambo mawili ambayo hayajafikia muafaka.
Aidha aliongeza kuwa mambo mawili ambayo hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili, ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance) huku la pili akilitaja ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari.
“Kwanza sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka sh. 10,000 hadi sh. 25,000 kwa daktari bingwa (Specialist), sh. 20,000 kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na sh. 15,000 kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.”
“Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.
Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya. Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale. Jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe sh. 3,500,000 wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.”
“Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya sh. 1,100,000 na 1,200,000 kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania sh. 3,500,000.”
“Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo,” alisema Rais Kikwete.