Pinda aitaka ALAT ikunjue makucha


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameitaka Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) iache kukaa kimya na badala yake ikemee uozo unaofanywa na watendaji kwenye Serikali za Mitaa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Julai mosi, 2012) wakati akifunga maadhimisho ya nane ya Siku ya Serikali za Mitaa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa Katiba ya ALAT, Jumuiya hiyo inao wajibu wa kuzisimamia Halmashauri kwa iliundwa ili kudumisha na kukuza maendeleo ya shughuli za Serikali za Mitaa Tanzania kwa kuondoa vikwazo na matatizo yote.
“Serikali za Mitaa zinakabiliwa na changamoto nyingi lakini kubwa nilizozianisha ni ukusanyaji mdogo wa mapato, usimamizi duni wa matumizi ya fedha na baadhi ya Halmashauri kushindwa kupata ruzuku ya maendeleo,” alisema.
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji mdogo wa mapato, Waziri Mkuu alisema uko chini licha ya Halmashauri nyingi kuonesha kuwa zingekusanya mapato na kuongeza vyanzo vya mapato.
“Taarifa zinaonyesha kumekuwepo udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Halmashauri. Vilevile, kuna usimamizi dhaifu wa mapato ambayo tayari yameshakusanywa… baadhi ya Halmashauri zimeshindwa kufikia viwango vilivyowekwa katika Makisio ya Bajeti zao za kila mwaka. Jitahidini mfikie walau asilimia 90 ya kile mlicholenga kukusanya,” alisisitiza.
Akitoa mfano alisema katika mwaka 2011/2012 hadi Mwezi Machi 2012 ukusanyaji wa mapato ya ndani (own source) ulifikia Asilimia 40.8 ya lengo ambalo liliwekwa la kukusanya shilingi Bilioni 350.5 “Nimeelezwa kuwa kiasi kilichokuwa kimekusanywa kilikuwa shilingi Bilioni 143 tu na hadi Juni 2012 makusanyo yalitarajiwa kufika shilingi Bilioni 200 kutokana na chanzo hiki ikiwa ni asilimia 57 ya lengo la mwaka.”
Alisema katika baadhi ya Halmashauri ukusanyaji mdogo unachochewa na udhaifu katika usimamizi wa mawakala wa ukusanyaji mapato, usimamizi dhaifu wa vitabu vya ukusanyaji mdogo wa mapato unasababisha Halmashauri nyingi kuendelea kutegemea Ruzuku kutoka Serikali Kuu na vilevile kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Napenda kusisitiza kwamba ukusanyaji thabiti wa mapato ni moja ya nguzo kubwa inayoonyesha uhai wa Serikali yoyote. Ninaamini ALAT itaacha kukaa kimya na badala yake iseme kitu kuhusu kasoro hizi zinazojitokeza,” alisema.
Kuhusu usimamizi wa fedha za Serikali, Waziri Mkuu alimtaka Mwenyekiti wa ALAT, Bw. Didas Masaburi na timu yake waende kukagua Halmashauri zilizoshindwa kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG).
“Mwaka 2007/2008 hati safi zilikuwa 90; mwaka 2008/2009 hati safi 97, mwaka 2009/2010 hati safi 81; na mwaka 2010/2011 hati safi zilikuwa 100. Aidha, Hati zisizoridhisha zimepungua kutoka Hati 43 mwaka 2007/2008 hadi Hati 33 mwaka 2010/2011…. Mwenyekiti wa ALAT mwende mkakague hizi Halmashauri zenye hati chafu na muwaulize kulikoni!” alisistiza.
Alisema wakijenga tabia ya kukagua Halmashauri na Manispaa watasaidia kupunguza kasoro nyingi zinazoibuliwa na CAG na kumfanya CAG akose kazi ya kufanya.
Kuhusu ruzuku, Waziri Mkuu alisema Halmashauri nne za Wilaya za Rombo, Kishapu, Bagamoyo na Kilosa hazikupata ruzuku kwa kushindwa kukidhi vigezo ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya Fedha, kutozingatiwa kwa Taratibu za Manunuzi, kupata Hati isiyoridhisha kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Serikali mwaka 2009.
Alizitaja Halmashauri nyingine tisa zilizoshindwa kupata Ruzuku ya Kujenga Uwezo (Capacity Building Grant) kuwa ni Rombo, Ulanga, Masasi, Newala, Tandahimba, Bukombe, Kilindi na Manispaa ya Kigoma Ujiji na Tabora.
“Vigezo nilivyovitaja hapo juu hivyo viko wazi na siyo siri. Inashangaza kuona kuwa zipo baadhi ya Halmashauri ambazo viongozi wake ni Wakurugenzi, Madiwani na Wenyeviti wa Halmashauri ambao ni wanachama wa ALAT lakini, zinashindwa kukidhi vigezo hivyo na hivyo kukosa fedha za Ruzuku ya Maendeleo. Sioni sababu za msingi kwa Halmashauri kushindwa kukidhi vigezo hivyo na wala ALAT kuendelea kukaa kimya wakati wananchi wanakosa fedha za maendeleo,” alisema. Waziri Mkuu anaondoka Mwanza kesho asubuhi (Jumatatu, Julai 2, 2012) kurejea Dodoma kuendelea na kikao cha Bunge.