MAMLAKA ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) yatapanuliwa katika siku za usoni kushughulikia pia kesi za makosa ya jinai zikiwemo za mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu.
Msajili wa Mahakama hiyo Profesa John Ruhangisa aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) katika mahojiano maalum kwamba mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa maelekezo ya kikao cha hivi karibuni cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“ Ni kweli kwamba upanuzi wa mamlaka ya Mahakama hii yatahusisha pia mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na hii ni kwa mujibu wa maelekezo ya Kikao cha Wakuu wa Nchi wananchama. Inamaanisha kwamba Mahakama hii itakuwa na uwezo wa kushughulikia mashitaka kama vile ya mauaji ya kimbari na mengine kama vile ya watuhumiwa wa Kenya ambayo kesi yake sasa ipo mbele ya ICC( Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai),” Profesa Ruhangisa alifafanua.
Vyote viwili, Mahakama na Afrika Mashariki vina majaji wenye uwezo wa kushughulikia kesi za aina hii, alisema katika mahojiano ambayo yatachapishwa hivi karibuni. Mahojiano hayo yaliyofanyika katika lugha ya Kiingereza, pia yatapatikana katika lugha za Kiswahili na Kifaransa kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya kanda.
Lakini alikiri pia kwamba kuna vikwazo. Alisema upatikanaji wa rasilimali watu na fedha za kugharimia upanuzi huo ni miongoni mwa changamnoto iliyopo. Mambo haya yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi kwanza, aliongeza.
Alifafanua kwamba ili mahakama iweze kushughulikia kesi za jinai kunahitajika kuanzishwa kwa idara mbalimbali ikiwa ni pamoja na za mwendesha mashitaka, upelelezi, ulinzi wa mashahidi na magereza.
“ Inawezekana kiufundi na kiutekelezaji lakini masuala mengi yanahitajika kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuelekea rasmi upande huo,” alishauri.
Iwapo EACJ itafanikiwa kufikia hatua hiyo ya upanuzi wa mamlaka yake kushughulikia kesi za jinai, itakuwa imelamba ‘bingo’ ya hatma yake ya kuweza kushughulikia matatizo yake yenyewe katika kanda ya EAC. Na pia kamwe kutoshuhudia tena mauaji yaliyotokea Rwanda na Kenya.
Hivi sasa EACJ inashughulikia mashauri yanayohusu zaidi madai.