TIMU ya Mara imeuanza vibaya mwezi Julai baada ya leo asubuhi kupata kipigo cha mabao 5-0 mbele ya Dodoma katika mechi ya michuano ya Copa Coca-Cola iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Dodoma ambayo hiyo ni mechi yake ya nne mfululizo kushinda katika kundi hilo la C ilipata mabao yake kupitia kwa Vicent Tarimo aliyefunga dakika ya kwanza, Japhet Lunyungu (dakika ya sita), Ayoub Khalfan (dakika ya 65 na 89) na Abdul Madwanga (dakika ya 67).
Kundi A limeshuhudia Ruvuma ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Kusini Pemba katika mchezo uliofanyika leo asubuhi (Julai Mosi mwaka huu) kwenye Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na Sunday Leonard (dakika ya nne) na Shanely Michael (dakika ya 44). Abdulatif Salim aliifungia Kusini Pemba dakika ya 90.
Nazo Iringa na Tanga zimetoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kundi B iliyochezwa Uwanja wa Tamco ulioko mkoani Pwani. Kagera imeitambia Tabora baada ya kuifunga mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam. Athuman Kassim na Shabani Ramadhan ndiyo walioifungia Kagera dakika ya sita na 88.