Serikali itazame upya mfumo wa ufundishaji


Na mwandishi wetu
SERIKALI imeshauriwa kutizama upya sera ya elimu na kubadili mfumo wa ufundishaji mashuleni hatua ambayo itasaidia kukabiliana na tatizo la ongezeko la watoto wanaomaliza elimu ya msingi huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.

Ushauri huo ulitolewa jana na ASkofu wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Dkt.Martine Shao wakati akifungua kongamano la walimu wa shule na vyuo vya Montesori kutoka mikoa yote ya Tanzania lililofanyika mjini moshi ambapo alisema ongezeko la wanafunzi kumaliza elimu ya msingu huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika linazidi kurudisha nyuma kiwango cha elimu hapa nchini.
Alisema wanafunzi kumaliza elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma na kuandika inatokana na mazingira yasiyo mazuri katika shule za serikali kuanzia ngazi za awali hadi sekondari hivyo umefika wakati sasa kwa serikili kutafuta njia ya kukabili tatizo hilo kabla halijaleta madhara makubwa.
“Ni wakati sasa kwa serikali kutazama suala la elimu kwa upya kwani taarifa za wanafunzi kumaliza elimu ya msingi huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika zinaumiza sana kwani jambo hili haliwaingii watu wengi akilini kwamba mwanafunzi amesoma miaka saba na ametumia fedha nyingi za wazazi halafu anamaliza hajui kusoma,kuandika wala kuesabu hii ni hatari sana kwa hapo baadae na ni lazima serikali itafute suluu mara moja”alisema Dkt. Shao.
Aidha Dkt. Shao alisema ni vema serikali ikaona umuhimu wa kuwekeza katika elimu kutokana na kwamba katika nchini ya Tanzania kumekuwepo na rasilimali nyingi ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu wachache kujinufaisha binafsi ili hali shule za serikali hazina vifaa vya kufundishia, walimu wa kutosha wala maabara licha ya serikali kusema inataka kuinua kiwango cha sayansi.

Dkt. Shao alisema Tanzania imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa mambo yasiyo na maana na kwamba endapo raslimali za nchi kama madini yangetumika vizuri na kuona umuhimu wa elimu wanafunzi mashuleni wasingekosa madawati,vitabu , walimu wa kufundisha wala maabara.

Katika hatua nyingine Askofu shao alisema hali iliyopo sasa ya ufisadi,rushwa, dhuluma na ukatili katika taifa inatokana na watanzania kutokuwa na maadili hivyo ni vema watoto wakaandaliwa vizuri toka katika shule za awali ili kuweza kumaliza matatizo hayo.
Nao baadhi ya walimu walioshiriki katika kongamano hilo walisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mishahara midogo pamoja na wao kutothaminiwa hivyo kuiomba serikli kuona umuhimu wa kuwaajiri na kuwalipa stahiki zao kama watumishi wengine hapa nchini.