Hali ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka ni mbaya na sasa madaktari wanatafuta Dola za Marekani 40,000 (Sh. milioni 63.07) ili aweze kupelekwa nje ya nchi kwa wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Edwin Chitage, alisema hayo jana kwenye hospitali ya Taasisi ya Mifupa (MOI), alikolazwa Dk Ulimboka wakati madaktari bingwa wakitoa tamko la kutangaza mgomo wa madaktari bingwa wote wa mkoa wa Dar es Salaam, kuanzia jana.
Tamko hilo limefuatia madaktari hao kukutana jana katika kikao chao maalumu na kuitaka serikali ieleze mustakabali wa maisha yao kutokana na hofu waliyonayo, kufuatia daktari mwenzao kufanyiwa kitendo hicho cha kinyama.
Dk. Chitage alisema kuwa, wameamua kutafuta fedha hizo ili kuokoa maisha ya mwenzao ambaye hali yake imebadilika ghafla baada ya figo zake kushindwa kufanya kazi.
Hadi jana kiasi cha Sh. milioni 40/- kilikuwa kimepatikana kutokana na michango iliyochangwa na madaktari.
Aidha, wamewaomba madaktari na wadau wengine walioguswa na tukio hilo kujitokeza kuchangia fedha hizo ili kuokoa maisha ya daktari mwenzao.
Kwa mujibu wa daktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Catherine Mung’ong’o, mgomo huo wa madaktari bingwa utaendelea mpaka hapo mwenzao atakapopona.
Alisema kutokana na hali ya mwenzao kubadilika ghafla, wakati wowote kuanzia sasa wanatarajia kumpeleka nje ya nchi kupitia Nairobi, Kenya.
“Hali yake imebadilika tofauti na jana (juzi), wakati tunatafuta fedha hizi, tunatarajia kumpeleka nje ya nchi ili kufanyiwa vipimo vingine ambavyo hapa nchini havipo,” aliongeza.
Daktari huyo aliongeza kuwa, wamefadhaishwa na kitendo hicho na wanalaani unyama aliofanyiwa daktari mwenzao.
MADAKTARI WALIOSIMAMISHWA
Katika hatua nyingine, madaktari hao bingwa walisema wamesikitishwa na kitendo cha serikali kuwasimamisha na kuwanyima mshahara madaktari kinyume cha taratibu kufuatia suala hilo kuwa mahakamani.
“Bunge lilisema linasubiri tamko kutoka mahakamani iweje hatua zianze kuchukuliwa wakati suala hili halijatolewa hukumu na mahakama, tunawataka wenzetu warudishwe kazini haraka,” alisema.
Alisema hata wabunge wanapojaribu kujadili suala hilo bungeni huzuiwa na Spika wa Bunge kwa madai kuwa bado lipo mahakamani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Kidjo- Bisimba, alisema inashangaza hatua kuchukuliwa kabla ya mahakama kuamua.
“Serikali haijielewi iweje uchukue hatua kabla ya mahakama kutoa tamko ina maana Waziri Mkuu alivyosema liwalo na liwe ndio wanatimiza haya wanayoyafanya sasa ya kufukuza madaktari, wataalamu sasa wanagoma itakuaje, serikali ndio inasababisha mgogoro”, aliuliza.
WAUGUZI-SERIKALI ICHUNGUZE
Chama cha Wauguzi tawi la Taasisi ya Mifupa (MOI), kimesema kimesikitishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dk. Ulimboka na kuiomba serikali ifanye uchunguzi wa kina na wa haraka ili kubaini wote waliohusika na sheria ichukue mkondo wake kwa waliohusika.
Katika hali isiyo ya kawaida jana MOI, ilifunga milango mikuu ya kuingia ndani ya jengo hilo na kusababisha ndugu kuacha vyakula vya wagonjwa wao kwa walinzi.
LANGO KUU MOI LAFUNGWA
NIPASHE Jumamosi jana ilishuhudia lango kuu la kuingilia kwenye jengo hilo likiwa limefungwa huku walinzi wa hapo wakiwa ndani na nje kuhakikisha ulinzi unakuwepo na hakuna mtu yeyote anayeingia zaidi ya madaktari.
Mmoja wa mwananchi aliyeleta chakula kwa mtoto wake ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuhofia mgonjwa wake kutohudumiwa, alisema kuwa, ameshangaa baada ya kufika hapo na kutakiwa na walinzi aache chakula mlangoni.
“Nimefika hapa lakini cha ajabu walinzi wale wameniambia niache chakula kwao na siruhusiwi kuingia ndani kumuona mgonjwa wangu, jamani serikali iliangalie suala hili, wananchi tunateseka kwa sababu tu wamegoma kuyasikiliza madai ya madaktari,” alisema.
Daktari mmoja aliyekutwa kwenye taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa, inadaiwa wakati wa tukio kifaa kilichotumika kung’oa kucha na meno na kubinywa sehemu za siri kilikuwa ni koleo.
Kadhalika alisema kuwa, ameshangazwa na kitendo cha serikali kumteua mmoja wa watuhumiwa kuwepo kwenye tume inayochunguza tukio hilo.
Habari zilizofikia gazeti hili na kudhibitishwa na daktari huyo, zimesema kuwa, siku ya tukio, Dk. Ulimboka alitaka kuuawa kwa bastola lakini kutokana na kuzimia ghafla baada ya kipigo, watuhumiwa walidhani ameshakufa.
Baadhi ya watu waliomtembelea ni pamoja na Mwenyekiti Mtendaji wa Makamapuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, Hellen Kihjo Bi-Simba na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini, (Tamwa), Ananalia Nkya.
MADAKTARI WATAKIWA KURUDI KAZINI IFIKAPO JULAI 2
Kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea nchini wa kuishinikiza serikali itekeleze madai yao, baadhi ya hospitali zimeanza kuwachukulia hatua watumishi wake kwa kuwataka waandike barua ya kurejea kazini.
NIPASHE Jumamosi ilishuhudia matangazo katika Hospitali za MOI, Muhimbili na Amana ukiwataka madaktari kuandika barua ya kuwataka kurudi kazini ifikapo Julai 2, mwaka huu.
Matangazo hayo yalikuwa yamebandikwa katika ubao wa matangazo katika hospitali hizo na wakuu wanaoziongoza hospitali hizo kwa watumishi wote.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, baada ya kuandika barua hizo wametakiwa kusubiri maelekezo.
“Uongozi umepokea maelekezo kwamba watumishi ambao hawakuwepo kuanzia Juni 25, mwaka huu wanatakiwa kuandika barua ya kurejea kazini ipitie kwa Mganga Mkuu wa hospitali kupitia kwa Mganga Mkuu wa Manispaa kwenda kwa Mkurugenzi “imesema sehemu tangazo hilo na kuongeza:
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya madaktari wa hospitalini hapo waliokutwa wakiendelea na kazi, walisema kuwa, hatua iliyofikiwa hivi sasa itasababisha kuwepo kwa mkanganyiko kati ya madaktari waliogoma na wale wanaoendelea na kazi.
Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa, madhara ya mgomo huo ni makubwa kwa sababu, baadaye kutakuwepo na makundi mawili.
“Kwa kweli hali sio nzuri na hii itafanya waliogoma watuone sisi kama ni wasaliti kwao kwa sababu tunaendelea na kazi, lakini hata kwa wagonjwa wetu nao wamekuwa hawatuamini wanaona kama tunaofanya kazi hatufanyi kwa moyo,” alisema daktari huyo.
Aliongeza kuwa, upungufu wa madaktari kwa sasa umesababisha wale waliobaki kufanya kazi bila kupumzika.
Kwa mujibu wa muuguzi aliyekutwa wodi ya wanaume ya upasuaji hospitalini hapo alisema kuwa, toka juzi jumla ya wagonjwa watatu ndio waliopokelewa hapo na kwamba huduma zinaendelea kutolewa kwa wagonjwa kama kawaida.
WAGONJWA WAZUNGUMZA
Akizungumza na mwandishi mmoja wa wagonjwa wodini hapo, alisema huduma zinaendelea ingawa sio za kuridhisha.
Katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, baadhi ya madaktari wameeleza kuwa, hali ilipofikia imewakatisha tamaa ya kuendelea kufanya kazi na kwamba wapo tayari kwa lolote.
Mmoja wa madaktari hospitalini hapo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa, asilimia kubwa ya madaktari wenzake alioongea nao wamekiri kukata tamaa kuendelea na kazi hiyo.
“Mgomo ulipoanza baadhi ya huduma zilikuwa zinatolewa lakini baada ya Dk. Stephen Ulimboka kujeruhiwa, huduma zimesitishwa, hii ni aibu kwa serikali yetu, ” alisema mmoja wa madaktari ambaye hakutaja jina lake liandikwe gazetini.
Katika hospitali ya Mwananyamala, baadhi ya wananchi waliliambia gazeti hili kuwa, hospitalini hapo mgomo unafanyika chini chini.
Mwanamke aliyekutwa ndani ya hospitalini hapo ambaye ana mgonjwa aliyelazwa wodi namba nne, anayesumbuliwa na moyo, alisema kuwa, toka juzi wamekuwa wakipata lugha mbaya kutoka kwa wauguzi huku baadhi wakiwataka wawahudumie wenyewe wagonjwa wao.
“Mgonjwa wangu anapumulia mashine cha ajabu juzi asubuhi nimefika hapa na uji muuguzi akaniambia niuache watampa, mchana nilivyokuja na uji mwingine, niliukuta ule wa asubuhi haujatumika umechacha, nilipomuuliza muuguzi akaniambia nimnyweshe mwenyewe, hata dawa nilizoandikiwa kuzinunua hazijatumika kwa mgonjwa,” alisema mwanamke huyo ambaye ameomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Aidha, alisema kuwa, baada ya kauli hiyo, mfanyakazi mwingine wa kiume hospitalini hapo ndiye aliyetoa msaada kwake kwa kumuelekeza jinsi ya kumlisha mgonjwa kwa kutumia mpira.
Kwa upande wa hospitali ya Temeke NIPASHE Jumamosi ilikuta baadhi ya wagonjwa wakiendelea na huduma kupitia kwa watumishi ambao hawajagoma.
HINDU MANDAL YAZIDIWA WAGONJWA
Katika hatua nyingine, hospitali ya Hindu Mandal jana imelazimika kukataa wagonjwa baada ya kuzidiwa na kusababisha wale wanapelekwa hapo wakitoka hospitali za serikali kutopokelewa.
NIPASHE ilishuhudia jana saa tano asubuhi mgonjwa mmoja akirudishwa baada ya ndugu zake kufika hospitalini hapo na kuambiwa kuwa wodi zimejaa.
KAMBI YA UPINZANI YAMJIA JUU SPIKA
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imemjia juu Spika wa Bunge, Anne Makinda, ikidai kuwa amekuwa akitumia nafasi yake kuilinda serikali bungeni kwa kuzuia mjadala kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea nchini kote na kutekwa nyara kwa Dk. Steven Ulimboka, kwa kisingizio cha kuwapo kesi mahakamani inayohusu mambo hayo.
Mnadhimu wa Kambi hiyo, Tundu Lissu, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa kutokana na hilo, hawako tayari kuruhusu jambo hilo kwa kuwa linakiuka kanuni za Bunge.
Ili kuonyesha kuwa wako makini juu ya jambo hilo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema jana kuwa atatumia siku ya leo kuwasilisha hoja ya kutaka suala hilo lijadiliwe na Bunge.
Alisema iwapo hatua hiyo itakwama, watachukua hatua, ambazo zitakuwa ni ujumbe tosha.
Awali, Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema anashangazwa na hatua ya Spika Makinda kuilinda serikali bungeni wakati akijua wazi kuwa jambo lililopo mahakamani halihusiani na Jumuiya ya Madaktari Tanzania pamoja na kutekwa nyara kwa Dk. Ulimboka.
“Tangu jana (juzi), tukinyanyuka ili kuweza kutaka kupata ufafanuzi wa jambo hili Spika Makinda, amekuwa akituambia kaa chini hili jambo hili lipo mahakamani, kwa hakika anachokifanya ni kinyume cha kanuni za Bunge.
“Tunapata shida sana leo hii huwezi kusema jambo lipo mahakamani wakati huo huo serikali imekuwa ikiwafukuza madaktari kazini, uonevu hapana na tutatumia kanuni hizi hizi leo hii kuweza kufikisha ujumbe juu ya jambo hili ili liweze kujadiliwa na Bunge,” alisema Lissu.
Akizungumzia jaribio la mauaji dhidi ya Dk. Ulimboka, Lissu alisema inahitajika tume huru kuundwa ili kuchunguza suala hilo.
“Tume hiyo tunahitaji Mwenyekiti wake awe jaji wa Mahakama Kuu au Rufaa na wajumbe wake watoke taasisi zinazoaminika mbele ya jamii kama Chama Cha Wanasheria wa Tanganyika.”.
VIONGOZI WA DINI WALAANI
SIKU tatu baada ya kutekwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Steven Ulimboka, viongozi wa dini nchini wamelaani kitendo hicho, huku wakiinyoshea vidole serikali.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, alisema alitamani sana kuingilia kati mazungumzo kati ya serikali na madaktari hao.
“Binafsi nilikuwa na mpango wa kukutana na viongozi wa madaktari hao kuzungumza nao ili warejee kazini hasa ikizingatiwa kuwa kazi hiyo ni ya wito huku mazungumzo ya amani na serikali yakiendelea.
Ningepata fursa ya kuzungumza nao, Mungu angejalia huenda haya yaliyotokea yasinge tokea,” alisema Askofu Dk. Mokiwa.
Akizungumza kwa tahadhari ya kutomnyooshea kidole mtu au taasisi kuhusika na tukio la Dk. Ulimboka, Dk. Mokiwa alisema inasikitisha kuona watu wakidai vitu vya msingi lakini wananyamazishwa kwa njia zisizo halali.
Hata hivyo, alisema kuwa hata kama kuna vitu vya msingi vinavyodaiwa na madaktari hao, njia ya kutumia mgomo waliyotumia ni mbaya kwani wangeendelea na njia ya mazungumzo tu na serikali.
Alisema wale waliohusika na tukio hilo, Mungu amewaona na wale waliofanya mgomo kwa kukomoana tu, Mungu pia amewaona.
“Serikali inalazimika kuwasikiliza madaktari hao vitu vyao vya msingi wanavyodai. Hatuwezi kujengeana utamaduni wa kufumbiana midomo kwa kupigana…” alisema Askofu Dk. Mokiwa na kusisitiza kuwa yuko tayari kuzungumza na pande zote katika kuhakikisha madaktari hao wanarejea kazini.
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Issa Shaaban Simba, alisema amesikitishwa sana na tukio alilofanyiwa daktari huyo. Alisema kama watu wanadai vitu vyao vya msingi na nchi ikafikia hatua hiyo, itakuwa ni nchi ya hatari sana.
“Nalaani sana kitendo hiki, wahusika wasakwe hadi wapatikane na kuchukuliwa hatua,” alisema.
Alfajiri ya Jumatano wiki hii, katika msitu wa Mwabwepande uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, wasamaria wema walimuokota Dk. Ulimboka akiwa hajitambui na kisha kukimbizwa katika hospitali ya Muhimbili ambako anaendelea kupatiwa matibabu kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
BUGANDO HUDUMA ZIMEDORORA
WAKATI Hospitali ya Rufaa ya Bugando imetekeleza agizo la serikali la kuwatimua madaktari walio katika mafunzo ya vitendo ambao wanashiriki mgomo ulioenea maeneo mbalimbali nchini, Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk.Charles Majinge amekiri huduma za matibabu hospitalini hapo kudorora.
Aliwaambia waandishi ofisini kwake jana kuwa, Dk.Majinge alisema kwamba jumla ya madaktari 63 walio katika mafunzo kwa vitendo katika hospitali hiyo na ile ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure wameondolewa na kurejeshwa wizarani kutokana na kushiriki mgomo.
Alisema kwamba kwa kiasi fulani hatua hiyo imeathiri huduma za matibabu licha ya kwamba madaktari bingwa waliopo hospitalini hapo wanajitahidi kufanya kazi zilizokuwa zinafanywa na madaktari hao waliogoma.
Kwa mujibu wa Dk.Majinge, hadi sasa madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa njia ya vitendo ambao wametimuliwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando ni 47 na kwamba wamerejeshwa wizarani kwa maelekezo ya serikali.
KCMC HALI TETE
Hali ya utoaji huduma katika hopitali ya rufaa ya KCMC, mjini Moshi, imezidi kuwa tete, kutokana na wagonjwa kupata huduma kwa kusuasua huku wahudumu wa afya na wauguzi wakilemewa na mzigo mkubwa.
Taarifa kutoka ndani ya hospitali hiyo zinaeleza kuwa wauguzi nao wamelemewa na mzigo, ambapo madaktari wanaofanya kazi ni wale ambao kwa imani zao za kidini na raia wa nje hawaruhusiwi kugoma ndio wanaohudumia wagonjwa.
Hata hivyo, idadi ya wagonjwa imepungua sana na baadhi ya wodi kuwa wazi, kutokana na wagonjwa wengi walioonekana kuwa na nafuu kuruhusiwa kuondoka hospitalini humo tangu mwanzo wa mgomo, huku kukiwa hakuna huduma kwa wagonjwa wa nje.
Mmoja wa madaktari aliye kwenye mgomo, alisema kwa ujumla hali si nzuri kwani hakuna madaktari na wagonjwa wachache waliopo wodini hawapati huduma inavyotakiwa, wanje ndio kabisa kliniki zote zimefungwa, kwani madaktari wachache sana ndio wanaendelea na kazi na wanaelekea kulemewa na mzigo.
MOROGORO YALAANI ULIMBOKA KUPIGWA
Baadhi ya wananchi Mkoa wa Morogoro, wametoa maoni yao kuhusiana na kitendo cha kutekwa na watu wasiojulikana na kumpiga na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka.
Ally Saleh mkazi wa Kihonda alilaani kitendo hicho kilichofanywa na kueleza kuwa ni cha kinyama huku akihusisha kuwa lazima kitakuwa na mkono wa serikali kwa nia ya kutaka kuwavunja nguvu madaktari hao ambao wameonyesha msimamo wao katika kutetea maslahi yao.
Naye Esther Mhina, ambaye ni mmoja wa wanachama wa mtandao unaojihusisha na kusaidia watu wenye ulemavu, alisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha jinsi gani nchi isivyokuwa na demokrasia na utawala bora watu ambao wanadai maslahi yao wanafanyiwa vitendo vya kinyama.
Alisema kuwa suluhisho la vitendo hivyo ni wananchi kuindoa serikali iliyopo madarakani ambayo inaongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwakuwa imekuwa ikishindwa kusaidia watalaam wake pamoja wananchi na badala yake imekuwa ikiwaneemesha vigogo wake ambao kila kukicha wanakwiba fedha .
Taarifa hii imeandaliwa na Romana Mallya na Beatrice Shayo, Dunstan Bahai,
Dar es Salaam, Muhibu Said, Dodoma, George Ramadhan, Mwanza, Salome Kitomary, Moshi.
CHANZO: NIPASHE