Wabunge Dodoma wafagilia huduma za Vodacom

Vodacom katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wazidi kufurahia huduma za malipo ya baada kwa wateja mmoja mmoja za kampuni ya Vodacom inayotambulishwa kwao mjini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wabunge hao kuzidi kufurahia huduma bora za mtandao huo nchini.

Wabunge wameonekana kupendezewa na huduma hiyo na hivyo kujiunga nayo katika zoezi maalum linaloendeshwa na maofisa wa Vodacom katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma lililoanza mwishoni mwa wiki.

Baadhi ya wabunge waliopata maelezo ya huduma hiyo ya malipo ya baada wamesema inatoa urahisi katika matumizi na malipo huku ikitoa uhakika wa mawasiliano hata katika maeneo ambayo mteja huweza kujikutakatika mazingira hasa ya mbali na miji.

“Kutokana na shughuli zetu kuna wakati tunakuwa maeneo ya vijijini kabisa huku mahitaji ya mawasiliano yakiwa ni ya lazima kwa wakati wote hivyo huduma hii inarahisisha mawasiliano kwa kuwa na uhakika wa kutoishiwa salio,” Alisema Mbunge wa Tabora Mjini, Alhaj Ismail Aden Rage.

Baadhi ya wabunge wamesema mifumo hiyo ndio inayotakiwa kuhimizwa ili kuendana na maendeleo ya teknolojia ya simu za mkononi na kupunguza utamaduni wa malipo ya kabla huku wakiipongeza Vodacom kwa kubuni huduma hiyo kwa wateja mmoja mmoja tofauti na utamaduni uliozoeleka wa huduma hizi kutolewa kwa utaratabu wa makampuni ama taasisi.

Kupitia mfumo wa malipo ya baada kwa mteja mmoja mmoja Vodacom huwawezesha wateja wake kupitia njia mbili za Choice na Voda jaza. Pamoja na huduma hiyo wabunge hao wamevutiwa na kuhamasika pia na huduma za intaneti za simu za mkononi za Black Berry yaani BIS ambazo wengi wa wabunge wamejiunga nayo.

Huduma ya Vodacom malipo ya baada kwa mteja mmoja mmoja inapatikana kwa kiwango cha kuanzia sh. 50,000 kwa huduma ya Vodacom Jaza pamoja na Vodacom choice ambayo haina ukomo wa gharama.