Simanjiro walia na Serikali

WANANCHI wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamelalamikia kitendo cha kuhamishwa kwa mkuu wa wilaya hiyo Bw. Peter Toima aliyeteuliwa mwezi May mwaka huu na kusema kuwa kitendo hicho kimetokana na shinikizo la Kisiasa hivyo kama serikali haitakuwa makini katika hilo wote watakihama chama cha mapinduzi na kuhamia chadema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika jana katika kijiji cha Narakauo kata ya Loiborsiret wilayani humo wananchi hao walisema mkuu huyo ambaye aliapishwa Mei 17 mwaka huu na kuripoti katika wilaya hiyo alihamishwa Jun 11 hali ambayo imewaumiza sana kutokana na kwamba kufika kwake waliona ndiyo mwisho wa matatizo yao ambayo yanawakabili kwa muda mrefu pasipo msaada wowote.
Akizungumza mmoja wa wazee wa kimila waBw. Peter Toima alisema katika wilaya hiyo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uporaji wa Ardhi kiholela,ukosefu wa maji safi na salama,ukosefu wa shule pamoja na ukosefu wa barabara jambo ambalo waliamini kabisa kuwa kufika kwa mkuu huyo Peter Toima ingekuwa ni mwisho wa matatizo yao.
“Tulifurahishwa sana na uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambapo aliamua kutuletea Peter Toima katika wilaya ya Simanjiro ambaye hapa ni nyumbani kwake alikozaliwa na anayafahamu vizuri matatizo yanayotukabili, na tuliona kabisa kuwa atakuwa mmoja wa viongozi ambaye atayatatua matatizo yetu kwani kwa sasa kwakweli hakuna viongozi katika wilaya hii hata wale ambao tumewachagua leo wanatuona kama wanyama pori na daraja lao la kuyafikia mafanikio huku sisi tukiendelea kutaabika kwenye jangwa lisilo na msaada” alisema Bw. Kunga.
Alisema kuhamishwa kwa mkuu huyo kumetokana na shinikizo la baadhi ya wanasiasa katika wilaya hiyo ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhujumu rasilimali zilizopo wilayani humo ikiwa ni pamoja na ardhi hivyo kuogopa kuwa endapo mkuu huyo atabaki katika wilaya hiyo angeyafichua maovu yao na kuwaweka mahala pabaya kisiasa na hata katika Nyanja nyingine.
“Mei 17 tulishuhudia kuapishwa kwa DC mpya wa wilaya hii Peter Toima Pale Babati,kitendo hiki kilitufurahisha sana lakini Mwezi Jun 11 ilitangazwa kuwa si DC tena Simanjiro na badala yake anakwenda wilaya mpya ya Kakonko mkoani Kigoma,hali hii ilituumiza sana wanasimanjiro na tunashangazwa na Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Taifa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Kikwete kubadilisha maamuzi yake ambayo alikuwa ameyapanga kwa shinikizo la baadhi ya wanasiasa katika wilaya hii,yaani kumbe hata Rais anaweza kudanganyika?alihoji mwananchi huyo.
Akizungumza Bw.Lemayani Peshutu ambaye naye ni Legwanani alisema wilaya ya Simanjiro imesahaulika sana katika huduma mbalimbali za kijamii na kimaendeleo ikiwemo elimu,Afya,Maji na hata miundombinu,hali ambayo imesababisha wananchi kuishi katika mazingira magumu kama watoto yatima wasio na mama,Baba wala msaada wowote.
Alisema pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali,pia wapo watu ambao wamevamia misitu katika wilaya hiyo na kuharibu vibaya vyanzo vya maji hali iliyosababisha kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama na kwamba wametoa malalamiko hayo katika ngazi husika ikiwemo za wilaya pasipo mafanikio yoyote.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Leiborsiret wilayani humo Bw.Ezekiel Lesenga alisema moja ya mambo ambayo Rais Kikwete aliyapa kipaumbele wakati anaingia madarakani mwaka 2005 ni Kilimo Kwanza lakini katika wilaya hiyo hawajawahi kuona pembejeo,pawatila wala ruzuku za mifugo ingawa wamesikia kuwa ruzuku hizo zipo licha ya kwamba asilimia 80 katika wilaya hiyo ni wafugaji.
Alisema jambo lingine lililopewa kipaumbele na lipo katika ilani ya chama cha mapinduzi ni kila kata iwe na shule ya Sekondari lakini katika kata ya Leiborsiret hakuna sekondari na waliwahi kuchanga sh. Mil. 6o kwenye harambee iliyoongozwa na makamu wa rais wakati huo Dkt. Ally Muhamed Shein kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo lakini cha kushangaza na kusikitisha ni kwamba shule hiyo haijakamilika hadi sasa na waliwasilisha malalamiko wilayani na wilaya kukiri kuwepo kwa suala hilo pasipo kuchukua hatua zozote huku wananchi wakiendelea kutaabika na watoto wakikosa elimu bora.
Kufuatia hali hiyo wananchi hao wamemuomba Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Kikwete kufika katika wilaya hiyo ili kuweza kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi haraka iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwarudishia mkuu wa wilaya Peter Toima ambaye wanaamini kabisa kuwa atakuwa chachu ya maendeleo na mmoja wa viongozi wapigania haki za wananchi na mwenye kukemea uovu.
Walisema kama Rais aliweza kuwasikiliza watu wachache waliofika na kumlilia na kuamua kumuhamisha mkuu huyo ni vema pia akasikiliza halaiki ya wananchi wa simanjiro, na kutishia kwamba endapo rais hatawasikiliza watahamasishana na kukimaha chama cha mapinduzi na kwenda kwenye chama chochote cha siasa ambacho kitaweza kuwasaidia hata kwa miaka kumi ijayo lakini kiwe kimeonyesha juhudi.
“Wananchi Simanjiro timesherekea miaka 50 ya uhuru tukiwa malimbukeni,sasa tunamuomba Rais aje asikilize kilio chetu, na endapo rais hutatusikiliza sisi halaiki ya watu, na umeweza kuwasikiliza watu wachache tunakuhakikishia kuwa tutakihama chama cha CCM kwani tumechoka kukaa katika janga hili la mateso lisilo na msaada” alizungumza kwa uchungu Bi.Elizabeth Lucas na kuongeza kuwa Simanjiro wakina mama,watoto na hata wazee wote wanalia,hivyo kama simanjiro ni sehemu ya Tanzania ni vema Rais akafika kuwasikiliza .