Sakata la Mgomo wa madaktari lachukua sura mpya, daktari atekwa ajeruhiwa vibaya

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka akiwa amejeruhiwa vibaya baada ya kutekwa juzi.

Na Mwandishi Wetu, Moshi

SAKATA la Mgomo wa madaktari unaoendelea nchini kote limechukua sura mpya baada ya watu wasiojulikana kumteka katibu wa chama cha madaktari Tanzania Dk. Steven Ulimboka na kumpiga kisha kumjeruhi vibaya na kwenda kumtelekeza hali ambayo imewaumiza madaktari wengi na kuwafanya kuongeza makali ya mgomo.

Katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyoko manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya madaktari zaidi ya 150 kusitisha kutoa huduma na kupita katika idara zote kuhamasisha mgomo kwa madai kuwa kitendo cha kiongozi wao kupigwa ni cha kinyama na kikatili hivyo hawawezi kukivumilia.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina madaktari hao walisema wamesikitishwa sana na kitendo cha mwenzao kupigwa na kwamba hawawezi kujua ni daktari yupi ambaye atafuata kupewa kipigo.

Madaktari hao walisema hawatakuwa tayari kufanya huduma yoyote na hata zile za dharura walizokuwa wanafanya hawataweza kuzifanya tena hadi pale ambapo itatokea au kutangazwa vinginevyo.

Kufuatia tukio hilo madaktari hao wamelaani vikali kitendo hicho na kuitaka serikali kutambua kuwa madaktari ni watu muhimu sana katika nchi hivyo wanapaswa kuheshimiwa.
Aidha madaktari hao walivitaka pia vyombo vya dola na usalama hapa nchini kutoa tamko haraka juu ya lililomsibu daktari mwenzao na kwamba wasipofanya hivyo watajua zaidi nini cha kufanya.

Walisema hawana nguvu tena ya kufanya kazi kutokana na kwamba usalama wao ni mdogo hivyo hawatakuwa tayari kufanya kazi zozote hadi pale ambapo itatokea vinginevyo.
“Tumesikitishwa sana na tukio hili la mwenzetu kuumizwa na hatutakuwa tayari kufanya huduma yoyote hata zile za dharura ambazo tulikuwa tunazifanya hatutaweza kuzifanya tena,” walisema.

Wakizungumza baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo walisema mgomo huo ni hatari sana, kutokana na kwamba wengi wao wametoka katika hospitali nyingine na kupewa rufaa ya kwenda hapo hivyo watakuwa katika wakati mgumu kama madaktari wataendelea na mgomo.

Akizungumza Bi. Halima Mohamedi kutoka CCP manispaa ya Moshi aliiomba serikali kushughulikia matatizo ya madaktari kwa haraka ili kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa.