TFF kuwakumbuka wapiga picha mashindano ya COPA COCA-COLA

Rais wa TFF, Sir Leodger Tenga

*Ngorongoro Heroes kujipima na Misri, Rwanda

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litawazawadia wapiga picha za magazetini watakaoripoti mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 ngazi ya Taifa yanayoendelea kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola na kushirikisha mikoa 28 yanafanyika viwanja vya Tanganyika Packers, Kumbukumbu ya Karume mkoani Dar es Salaam, na viwanja vya Tamco na Nyumbu mkoani.

Zawadi ya sh. 250,000 itatolewa kwa picha bora katika maeneo matatu; action picture, fair play picture na mpiga picha ambaye ameripoti matukio mengi ya mashindano hayo yanayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Washiriki wanatakiwa kuwasilisha picha zao zilizotumika (cuttings) ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Wakati huo huo; timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) itacheza mechi nne za kirafiki na timu za Misri na Rwanda kabla ya kuivaa Nigeria kwenye mashindano ya Afrika.

Ngorongoro Heroes ambayo kwa mara ya kwanza itakuwa chini ya kocha mpya Jakob Michelsen itaanza kwa kucheza mechi mbili za Misri zitakazofanyika Julai 3 na 5 mwaka huu, na baadaye Julai 14 na 16 mwaka huu dhidi ya Rwanda.

Mechi zote zitachezwa nchini, na kama ilivyo Ngorongoro Heroes, Misri na Rwanda nazo ziko kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi za kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Algeria.

Katika raundi ya kwanza, Ngorongoro Heroes iliitoa Sudan ambapo katika raundi ya pili imepangiwa Nigeria, na mechi ya kwanza itafanyika jijini Dar es Salaam, Julai 29 mwaka huu. Timu hizo zitarudiana wiki mbili baadaye nchini Nigeria.

Iwapo Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Nigeria, katika raundi ya mwisho itacheza na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Afrika Kusini.

ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A ya ukocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa vijana kutoka Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).

Moja ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya miaka 18. Ubingwa huo aliupata msimu wa 2005/2006.

Wakati huo huo; Ruvuma imeanza vizuri michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Kigoma mabao 2-0 katika mchezo wa kundi A uliofanyika leo asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Kigoma ambayo iliifunga Lindi mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa juzi, ilishindwa kufua dafu mbele ya Ruvuma na kuruhusu bao katika kila kipindi.

Mabao yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Edward Songo. Mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 34 wakati la pili alilipachika dakika ya 84.

Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na Morogoro zilitoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.

Mkoani Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tamco.