TFF yamtaja kocha mpya timu ya vijana

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtambulisha rasmi mbele ya waandishi wa habari kocha mpya wa timu za Taifa za vijana, Jakob Michelsen kutoka Denmark ambaye amechukua nafasi ya Kim Poulsen ambaye hivi sasa anainoa Taifa Stars.

Michelsen ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja alitambulishwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na kusema falsafa yake ni kama ile ya Poulsen ya kumiliki mpira na kushambulia muda wote wa mchezo.

Kabla ya kuja Tanzania, Michelsen alikuwa kocha wa timu ya daraja la kwanza ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A ya ukocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa vijana kutoka Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).

Moja ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya miaka 18. Ubingwa huo aliupata msimu wa 2005/2006.

Wakati huo huo; Ruvuma imeanza vizuri michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Kigoma mabao 2-0 katika mchezo wa kundi A uliofanyika leo asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Kigoma ambayo iliifunga Lindi mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa juzi, ilishindwa kufua dafu mbele ya Ruvuma na kuruhusu bao katika kila kipindi.

Mabao yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Edward Songo. Mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 34 wakati la pili alilipachika dakika ya 84.

Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na Morogoro zilitoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.

Mkoani Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tamco.