Na Mark Mugisha, EANA-Arusha
KUIMARISHA mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni njia pekee kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kujitoa katika mipaka iliyowekwa na wakoloni, Shirika moja linaloshughulikia amani na usalama, lenye makaoa yake makuu nchini Uganda limeeleza.
Msomi wa Chuo Kikuu cha Makerere na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuhamasisha Maendeleo na Uhifadhi wa Mazingira (ACODE), Dk. Arthur Bainomugisha alisema, migogoro ya mipaka katika kanda ya EAC inatokea kutokana na ukweli kwamba EAC haijafikia lengo lake la mtangamano.
Dk. Bainomugisha alitoa maoni hayo katika mdahalo mjini Kampala mwishoni mwa wiki ulioandaliwa na Taasisi ya kudhibiti Silaha Ndogondogo nchini Uganda (UANSA).
Mdahalo huo pia ulihitimisha maazimisho ya Wiki ya Dunia ya Vita dhidi ya Silaha Ndogondogo na Nyepesi (SALW) iliyoandaliwa na Sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na Taasisi ya Afrika Mashariki ya Kudhibiti Silaha Ndogondogo (EAANSA) na Shirika la Kiamtaifa la Misaada ya Maendeleo ya Ujerumani (GIZ).
“Mtangamano wa kanda utashughulikia migogoro yote ya aina hii kwa sababu wakati utafika ambapo alama za mipaka ya nchi haitakuwa na maana tena,” Dk. Bainomugisha alisema na kutoa mfano wa mgogoro wa mipaka kati ya Uganda na Kenya ambao karibu upelekee nchi hizo mbili kuimngia vitani juu umiliki wa kisiwa kidogo cha Migingo.
Msomi huyo pia alitoa wito wa kuimarisha utawala wa demokrasia akisema kuwa hatua hiyo huweka katiba ambayo huelezea ubadilishanaji wa madaraka kwa amani na kwa namna hiyo huzuia uwezekano wa kutokea hali ya mapinduzi ya kijeshi na migogoro ya umwagaji damu.
“Hakuna budi kuwepo pia uhamasishaji wa uhusiano kati ya raia na jeshi katika Afrika,” aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) nje ya mdahalo huo.
Naye Ofisa mmoja Mwandamizi wa Jeshi la Uganda, Luteni Kanali, Gordon Busigye alisema tatizo la uvujaji wa silaha haramu linatokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii nyingi katika kanda hiyo. Alikuwa anawasilisha mada kuhusu “Hatua ya Serikali dhidi ya Matumizi ya Nguvu ya Silaha.’’
“Baadhi ya wazazi na watu hawatoi ushirikiano wa kutoa taarifa juu ya kuwepo kwa silaha haramu kwa maafisa wa usalama kwenye maeneo wanayoishi. Hii hatimaye huongeza uhalifu wa kutumia bunduki,” Busigye aliwaeleza washiriki wa mdahalo huo uliohudhuriwa na wabunge, wanachama wa vyama vya kiraia na waandishi wa habari.