Na Shomari Binda, wa Binda News-Musoma
BARAZA Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, limeonya vikali kitendo cha Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Joyce Ndalichako cha kuwafelisha wanafunzi wa kidato cha sita somo la maarifa ya Uislamu na kudai kuwa kitendo hicho ni hujuma dhidi ya uislamu.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Maulana Ramadhan Said Sanze, wakati akizindua ushirika wa akiba na mikopo wa waislamu wa mji wa Musoma, unaojulikana kama kutayba SACCOS kwenye uwanja wa Mkendo mjini Musoma.
Sheikh Sanze, amewataka watu waliohusika kuwafelisha wanafunzi wa kiislamu katika somo lao la maarifa ya uislamu kuacha kufanya hivyo, kwani matokeo ya hujuma hiyo yanaweza kusababisha chuki, uhasama na matabaka miongoni mwa wananchi.
Alisema haiwezikani kwa wanafunzi kufeli katika somo lao tena kwa kiwango kikubwa na kusema kuwa kama hiko hivyo katika somop hilo itakuaje katika masomo mengine kama kemia, hisabati, Jografia pamoja na masomo mengine.
“Hii ni hujuma na sisi tutaendelea kumng’ang’ania Ndalichako katika jambo hili hadi aondoke katika nafasi hiyo kwa kuwa hali hii imetusikitisha na hatuwezi kukabiliana na hili na tunaomba jamii ituelewe madai yetu ni ya msingi katika ustawi wa jamii,” alisema shekh Sanze.
Kwa upande wake, Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini Sheikh Mussa Yusuf Kundecha, amewataka waislamu kuachana na kuchukua mikopo inayotoza riba kwani kufanya hivyo ni kumkosea mwenyezi mungu na kujiingiza katika dhambi kubwa.
Kundecha alisema uanzishaji wa Saccos ya kutayba inayoendeshwa kwa misingi ya dini Mjini Musoma itakuwa ni mkombozi kwa waislamu wote na wale wanaopinganana masuala ya riba kwa ni kitu ambacho kimekatazwa kwa msisitizo mkubwa na Mwenyezi Mungu.
Alisema dhamana kubwa katika kutayba saccos ni kuunda vikundi ambavyo vitakuwa na watu wanaofahamiana kwa shughuli zao na maeneo wanayoishi na hakuna masuala kutozana kiasi chochote cha pesa ili kupata nafasi ya kujiunga.
Kundecha aliongeza kuwa Waislamu wanaweza kujikomboa kwa kujiwekea fedha kidogo kidogo na kuacha kujiingiza katika mikopo ambayo imekatazwa katika dini na kusema kuwa mikopo yenye riba imekuwa ikileta matatizo mbalimbali katika jamii ikiwemo kuuziwa thamani za nyumbani na kuacha familia zikiangaika.