Na Mark Mugisha, EANA, Arusha
MBUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Dora Byamukama wa Uganda, ameomba radhi kwa mpinzani wake na hatimaye mshindi wa kiti cha Spika wa Bunge hilo, Margaret Natongo Zziwa wa nchi hiyo pia kwa jinsi alivyoshiriki kwa namna isiyofaa katika uchaguzi wa nafasi hiyo mjini Arusha, mwanzoni mwa mwezi huu.
Spika Zziwa aliibuka mshindi katika raundi ya pili ya uchaguzi huo kwa kupata kura 33 dhidi ya Byamukama aliyeibuka na kura 12 ikiwa ni chini ya kura 18 alizopata katika raundi ya kwanza. Wabunge 45 kutoka nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walishiriki kupiga kura.
Kituo kimoja cha runinga nchini Uganda kimemnukuu Waziri wa Masuala ya EAC wa nchi hiyo, Eriya Kategaya akimwelezea Byamukama kuwa “hana maadili mema’’ kwa kumtupia shada la maua mezani kwake kama ishara ya kumpinga waziri huyo kwa kuripotiwa kuwa alikuwa anamfanyia kampeni Zziwa dhidi yake.
Mbunge Byamukama aliripotiwa pia kukataa kumshika mkono Zziwa kama ishara ya kidiplomasia ya kukubali kushindwa katika uchaguzi huo.
“Mimi ni mgeni katika ulimwengu wa kidiplomasia. Hata hivyo na kwa mara nyingine tena naomba radhi kwa mabaya yote yaliyojitokeza,” Byamukama, ambaye kitaaluma ni mwanasheria alieleza katika safu yake ya kila wiki kwenye gazeti la New Vision la Uganda lililochapishwa Juzi.
Katika safu hiyo pia mbunge huyo aliwashutumu wale ambao wanafikiria na kujenga dhana kwamba yeye amekosana na Spika mpya wa EALA kwa sababu tu walikuwa wanawania nafasi moja.
“Nitachukua hatua za ziada na kumpongeza mheshimiwa Margaret Zziwa kwa ushindi aliopata,’’ alisema. Wanawake hao, wote wawili ni wasomi wa ngazi ya juu na wametoka katika chama tawala nchini Uganda cha NRM.