NIDA waanza usajili wa raia na wageni Dar

Mkurugenzi Mkuu, Dickson Maimu

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeanza rasmi usajili kwa wananchi na wageni wote wanaoishi nchini Tanzania kihalalai kwa lengo la kuwapatia Vitambulisho vya Taifa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu, Dickson Maimu, zoezi hili litachukua siku 30, na litatanguliwa na kuandikisha wakazi wote waishio jijini Dar es Salaam katika daftari la makazi linalomilikiwa na Serikali ya kila mtaa.

Aidha usajili wa daftari la wakazi utasajili wakazi katika kila kaya, na maafisa usajili kwa kushirikiana na watendaji katika kila kitongozi au mtaa watapita nyumba kwa nyumba kufanya usajili huo kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi la ujazaji wa fomu za usajili kwa lengo la kutoa Vitambulisho

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa maafisa na watendaji watakaohusika na zoezi hili na kujitokeza kwa wingi katika usajili ili katika muda uliopangwa zoezi hili kukamilika na kutoa fursa ya usajili kuendelea katika mikoa mingine ya Tanzania ili kufikia malengo ya serikali zoezi hili kuwa limekamilika katika kipindi cha miaka miwili nchi nzima.

Shughuli hii imeanza rasmi tarehe 22/06/2012 hadi tarehe 21/07/2012 (kwa siku 30 tu). Walengwa katika zoezi la usajili ni watu wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.

Akifafanunua kuhusu mahitaji ya kuwa na vielelezo, Mkurugenzi huyo amesema ni muhimu kwa wananchi kujiandaa kuwa na vielelezo vitakavyo watambulisha ikiwa ni pamoja na cheti cha kuzaliwa, cheti cha ubatizo, cheti cha falaki au kadi ya kliniki vitakavyothibitisha tarehe ya mtu kuzaliwa, viengine ni kimoja wapo kati ya cheti cha elimu ya msingi, sekondari au chuo, pasi ya kusafiria, kadi ya mpiga kura, kitambulisho cha bima ya afya, kadi ya mfuko wa hifadhi ya jamii, au leseni ya udereva.

Amesema lengo ni kuwezesha Mamlaka kutambua wahisika ili kutoa kitambulisho kwa raia halali wa Tanzania, na kwa upande wa wageni ni nakala ya pasi ya kusafiria, na kibali cha kuishi nchini (resident permit). Kuwa na viambatanisho kutasaidia mtu kutambulika kwa haraka na kuchukua muda mfupi kuwa amepata kitambulisho chake.

Amesisitiza zoezi hili ni bure halitakuwa na tozo yeyote, na fomu za usajili zitatolewa bure katika vituo vya uandikishaji vitakavyofunguliwa katika kila kitongoji/ mtaa. Mwombaji anaweza kupata maelezo zaidi katika Ofisi Kata na Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa zilizopo Barabara ya Kilimani, Kinondoni jirani na Ubalozi wa Ufaransa.