Na mwandishi wetu
Bunda,
WANANCHI katika jimbo la Bunda wamemshukuru Mbunge wa viti maalum (CCM) kutoka Mkoa wa Mara Esther Bulaya kwa kufatilia kwa karibu suala la malipo ya fidia kwa Wananchi wa jimbo hilo kwa kuachia maeneo yao kwa ajili ya kupisha utekerezaji wa mradi wa kutenga maeneo maalum ya uwekezaji (EPZ).
Wakizungumza na MTANZANIA Mjini hapa kwa nyakati tofauti Wananchi hao walisema tangu yalipotolewa malipo kwa baadhi ya Wananchi tangu mwaka 2010 kumekuwepo na ukimya siku za katikati lakini kupitia swali lililoulizwa na Mbunge huyo katika kikao cha Bajeti kinachoendelea Mjni Dodoma wanaamini malipo yao yatafanyika mwezi wa saba kama ambavyo aliahidi katika majibu yake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Gregory Teu.
Mmoja wa Wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Muheri Mgendi alisema anamshukuru Mbunge huyo kwa kufatilia suala hilo kwa karibu kama ambavyo aliwahidi alipotembelea Jimbo hilo katika uhamasishaji wa shughuli za Maendeleo.
“Nautambua ufatiliaji wa Mbunge Esther na naamini licha Naibu Waziri kutoa ahadi hiyo mbele ya Bunge kuhusiana na malipo hayo atafatilia kwa ukaribu zaidi kuhakikisha fedha hizo zinapatikana kwa wakati ili kila Mwananchi anayedai fidia aweze kulipwa,”alisema Mgendi.
Alisema wamepokea kwa mikono miwili majibu ya Naibu Waziri kupitia swali lililoulizwa na Mbunge huyo na kuomba kutokuwepo na uzungushaji zaidi katika utekelezaji wake kutokana na kusubili fidia hiyo kwa muda mrefu huku wengine wakishindwa kuendeleza maeneo yao mapya kutokana na kukosa fedha hizo.
Kwa upande wake Amosi Wambura alisema majibu ya Waziri huyo yasiwe ya kisiasa kwa kuwa Wananchi wanaodai fidia hizo wanasubili mwezi wa saba ufike ili waweze kupata malipo yao na kuendelea na shughuli nyingine za kimaendeleo na kuendeleza makazi yao mapya waiohamia.
“Unajua unapoahamia makazi mapya kuna kuwa na changamoto zake sasa tumeshindwa kukabiliana nazo kutokana na kutokuwa na pesa lakini tunaamini baada ya kupata malipo hayo tutaendelea vizuri na shughuli zetu za kila siku katika kujitafutia maendeleo yetu,”alisema Amosi.
Mbunge Esther Bulaya aliuliza swali Bungeni akitaka kujua wananchi waliobaki katika malipo ya fidia ya kuachia maeneo maalum katika shughuli za uwekezaji katika Jimbo la Bunda ni lini watalipwa malipo yao na kuendeleza maeneo yao mapya.
Katika majibu yake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Gregory Teu alisema kuwa tayari fedha iliyobaki kwa ajili ya malipo hayo imeshatengwa kiasi cha sh bilioni 1,042,852,910 na hazina na zinatarajiwa kuanza kulipwa kuanzia mwezi julai mwaka huu kwa wahusika 164 waliobaki.
Alisema kuwa malipo hayo yatakuwa ni awamu ya tatu baada ya kufanyika kwa awamu ya kwanza mwaka 2007 na awamu ya pili mwaka 2010 na kudai kuwa jumla ya wananchi 280 wanaostahili kulipwa watakamilishiwa malipo yao ya fidia kutokana na kuachia maeneo yao kwa ajili ya uwekezaji.