Jamii yahimizwa kufuatilia vyeti vya kuzaliwa mapema


Na mwandishi wetu
Musoma,

WAZAZI pamoja na walezi wametakiwa kuhakikisha wanafatilia vyeti vya kuzaliwa vya watoto mapema baada ya kuzaliwa kama inavyoelekezwa na kuacha tabia ya kuanza kufanya kazi ya kufatilia vyeti hivyo pale mtoto anapotaka kwenda chuoni au kupata ufadhiri wa kwenda kusoma nje ya Nchi.

Hayo yamesemwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Musoma Debora Makinga alipokuwa akizungumza juu ya kufatilia vyeti vya kuzaliwa mapema na umuhimu wake kutokana na Wananchi wengi kutokuzingatia hilo na baadae kuanza kuangaika pale wanapopata nafasi ya kufanya jambo fulani.

Alisema kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo na msungamano wa Wananchi katika ofisi ya msajili wa vizazi,vifo na ndoa wakifatilia vyeti vya kuzaliwa hususani kwa wale wanaotaka kwenda vyuoni na kudai kuwa huo si utaratibu mzuri na unaweza kumfanya mtu kukosa nafasi ya kwenda kusoma kutokana na kudharau kufatilia vyeti vya kuzaliwa mara mtoto anapozaliwa.

Makinga alisema Wazazi pamoja na walezi inabidi wabadilike na kuweka umuhimu wa pekee katika suala la kupata vyeti vya kuzaliwa vya watoto mapema bada ya kuzaliwa ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kujitokeza pale litakapo hitajika kufanyika jambo la msingi ambalo linahusu vyeti vya kuzaliwa.

“Hili nimekuwa nikilikumbusha mara kwa mara kupitia vyombo vya Habari juu ya umuhimu wa kupata mapema vyeti vya kuzaliwa lakini bado Wazazi na walezi wamekuwa hawazingatii na matokeo wanapokuja kufatilia na kukuta kuna majukumu mengine ya kiutendaji wamekuwa wakilaumu ofisi”,alisema Makinga.

“Wapo wengine licha ya kuelewa umuhimu wa cheti cha kuzaliwa wanashindwa kufatilia mapema na kuwa navyo na pale wanapopata nafasi ya kazi ama kutaka kujiendeleza zaidi kielimu ndipo wanapoanza zoezi la kufatilia cheti cha kuzaliwa,”aliongeza.

Alieleza msongamano unaojitokeza kwa sasa katika ofisi yake kuhusiana na kutafuta vyeti vya kuzaliwa umekuwa ukikwamisha kazi nyingine za kijamii na hivyo kuwaomba Wananchi pale zinapokuwa zinafanyika kazi nyingine wasilaumu bali wazingatie suala la kushughulikia suala la vyeti vya watoto mapema mara baada ya kuzaliwa.